Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ametangaza kuanza kwa kliniki maalum ya kushughulikia kero za wananchi, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kuimarisha usikivu na utoaji wa huduma kwa wananchi kwa vitendo.
Akizungumza leo Machi 2, 2026 jijini Dodoma, amesema Ofisi yake imetenga siku tatu kuanzia Machi 4 hadi 6 ambapo Taasisi zote za umma zitahusika moja kwa moja na wananchi kupokea na kutatua kero mbalimbali.
"Lengo ni kuwapa wananchi nafasi ya kueleza changamoto zao na kupata majibu na mwelekeo wa ufumbuzi kwa haraka, " amesema.
Amefafanua kuwa katika kipindi hicho, huduma kadhaa zitatolewa bila malipo, ikiwemo za afya kama upimaji wa hiari na utoaji wa damu, pamoja na huduma nyingine zitakazotolewa na Taasisi shiriki.
"Hatua hiyo inalenga kuisogeza Serikali karibu na wananchi na kupunguza mzigo wa kero zinazocheleweshwa kushughulikiwa, " amesisitiza
Ameeleza kuwa changamoto za wananchi huendelea kujitokeza, jambo linalohitaji ushiriki kamili wa Taasisi zote ili mpango huu ulete matokeo yanayotarajiwa na hivyo kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika siku hizo tatu ili kuwasilisha kero zao na kushiriki katika kupata suluhisho.
Vilevile, Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma amezitaka Taasisi za umma kutekeleza wajibu wao kwa weledi, ukarimu na maadili ya huduma kwa wananchi.
Amesema kaulimbiu awali ya “Kero yako, wajibu wangu” imeboreshwa na sasa itakuwa “Kero yako, wajibu wangu – Tabasamu na Samia”, ikiwa ni msisitizo wa utoaji wa huduma kwa heshima na moyo wa kujali.
Akizungumzia kwa upande wa wananchi wa pembezoni amesema utaratibu huo utaendelea ili kuwafikia wananchi wa maeneo yote kwa kuzingatia miongozo ya Serikali.
Aidha, ameitaja namba ya huduma bure ,0738877752 itakayowezesha wananchi kutuma ujumbe mfupi wa kero zao ili zipokelewe na kushughulikiwa.
"Kwa ujumla, kliniki hii inatarajiwa kuongeza uwajibikaji wa taasisi za umma, kuboresha utoaji wa huduma na kuimarisha imani ya wananchi kwa Serikali kupitia utatuzi wa changamoto kwa wakati, " ameeleza Senyamule

Social Plugin