Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DKT. MAULID ASISITIZA ITIFAKI NA TABIA NJEMA KWA VIONGOZI WA ELIMU


Mkutano Mkuu wa 12 wa Umoja wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri Tanzania Bara (REDEOA) umeendelea kufanyika jijini Arusha kwa siku saba tangu ulipofunguliwa rasmi Machi 2, 2026 na Waziri wa Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Profesa Riziki Shemdoe.

Mkutano huo unawakutanisha Maafisa Elimu pamoja na wadau wa sekta hiyo kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayolenga kuboresha utendaji na kuongeza matokeo chanya katika sekta ya elimu nchini.

Akiwasilisha mada kuhusu Itifaki na Tabia Njema, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), Dk. Maulid J. Maulid, amesema viongozi wanapaswa kuishi kwa kuzingatia misingi ya nidhamu, tabia njema na utii kwa sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia utendaji wa shughuli za kisekta.

Amesema kuzingatia itifaki na maadili mema kutaimarisha mahusiano kati ya wadau na wasimamizi wa sekta ya elimu na kusaidia kufanikisha malengo ya kisera yaliyowekwa na Serikali.

“Taswira njema ya utumishi wa umma hujengwa katika misingi ya nidhamu, tabia njema na uwajibikaji,” amesema Dk. Maulid.

Aidha, amesisitiza kuwa uimarishaji wa itifaki utaongeza weledi na uwajibikaji miongoni mwa viongozi wa elimu, hali itakayochangia kuleta ufanisi zaidi katika taasisi wanazozisimamia.

Amehitimisha kwa kuwataka viongozi hao kuwa mabalozi wazuri wa maadili na utaratibu katika maeneo yao ya kazi ili kuongeza tija na kuchochea maendeleo ya sekta ya elimu na Taifa kwa ujumla.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com