Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Ni saa mbili usiku katika kijiji cha Mlanga, Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma. Kimya kizito kinatawala. Ghafla, sauti ya "huu… huu… huu…" inapasua utulivu wa usiku.
Kwa baadhi ya watu ni sauti ya kawaida ya ndege anayewinda gizani. Lakini kwa wengine ni ishara ya mkosi, onyo la maafa au ujumbe kutoka ulimwengu usioonekana.
Dakika chache baadaye, milango ya nyumba inaanza kufunguliwa. Watu wanatoka wakiwa na vijiti vinavyowaka moto, marungu, mawe na hata chumvi ya mawe. Macho yao yote yameelekezwa kwenye mti mmoja.
Hakuna simba, chui wala nyoka.
Juu ya tawi ametua bundi.
Ndege huyo, ambaye kwa wakati huo alikuwa akitimiza jukumu lake la asili la kuwinda panya na viumbe wengine wanaoharibu mazao, ghafla anageuzwa adui wa kijiji. Anatupiwa mawe, anafukuzwa kwa moto na wakati mwingine huuawa.
Wanaofanya hivyo huamini wamezuia mkosi usiingie katika familia au kijiji chao.
Lakini swali linabaki: Je, kweli wameondoa mkosi, au wameondoa mmoja wa walinzi muhimu wa mfumo wa ikolojia?
Kwa miongo mingi, simulizi zinazomhusisha bundi na nguvu za giza zimeendelea kurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi. Kutokana na hali hiyo, ndege huyo amekuwa akiuawa au kufukuzwa bila ushahidi wa kisayansi unaothibitisha kuwa uwepo wake una uhusiano na mikosi inayodhaniwa na jamii.
Hofu hiyo imejenga mtazamo unaopingana na uelewa wa kisasa wa uhifadhi wa bioanuwai.
Bundi ameishi maisha ya kimya kisicho na mtetezi,hajawahi kuandika historia yake, hajawahi kueleza upande wake, na hajawahi kujibu hukumu ambazo jamii imemwekea.
Kila anapopaa au kutoa sauti, tafsiri tayari zimeandaliwa na akili za kurithishwa za binadamu.
Katika baadhi ya jamii, kuonekana kwake juu ya nyumba kunatafsiriwa kama ishara ya msiba au kuna ujumbe wa ajabu kutoka ulimwengu usioonekana. Lakini yote haya yanatokea bila ushahidi wa moja kwa moja, bali kwa urithi wa imani na hofu zilizojengwa kwa vizazi.
Mzee wa Kimila wa kijiji cha Chilonwa Dodoma ,Makunga Kudeli anakumbuka jinsi alivyokua akifundishwa kumtazama bundi kwa tahadhari.
“Tulikuwa tukiamini akilia karibu na nyumba basi kuna jambo baya litatokea,ilikuwa ni hofu tuliyojengewa tangu utotoni,” anasema.
Kauli yake inaonyesha jinsi jamii ilivyoweza kuunganisha sauti ya asili na tafsiri za kiimani, bila kutafuta chanzo cha kisayansi nyuma yake.
Anaeleza kuwa kwa muda mrefu, bundi amekuwa akibeba hukumu ambazo hazikuandikwa mahakamani yoyote, bali katika vichwa vya binadamu.
Naye Judith Maligaa anasema tangu utoto wake hadi sasa akiwa na miaka 84 akili yake inajua Bundi ni kivuli cha hofu, ishara ya mikosi na mjumbe wa maafa si kwa ushahidi wa uhalisia, bali kwa nguvu ya imani aliyorithishwa na babu yake Mzee Maligaa bila kuuliza mara mbili.
"Sauti ya bundi ikisikika basi tulikuwa tunatoka nje kumrushia vijinga vya moto na chumvi na asipoondoka tunamuua,"anaeleza
Katika safari hiyo ndefu ya tafsiri zisizo na uthibitisho, kiumbe huyu wa usiku amenyamazishwa zaidi kuliko kusikilizwa, ameogopwa zaidi kuliko kueleweka.
Lakini historia ya binadamu ina tabia moja ya ajabu huchelewa kumtendea haki yule aliyedhulumiwa na fikra zake mwenyewe.
Na huenda leo, kupitia uelewa unaoanza kuota polepole, tutashuhudia mwanzo wa marekebisho ya hukumu hiyo ya muda mrefu.
Huenda huu ni wakati ambapo pazia linaanza kufunuliwa, na macho yanaanza kuona kile kilichofichwa na hofu,kwamba nyuma ya sauti ile ya usiku, hakuna ujumbe wa maafa, bali sauti ya kiumbe anayefanya kazi yake ya asili kwa ukamilifu wake.
Mtaalamu wa wanyamapori kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania(TAWA) Beatus Maganja anasema bundi ni sehemu muhimu ya mfumo wa ikolojia.
Anasema,Bundi hudumisha uwiano wa mfumo wa ikolojia na ni miongoni mwa wawindaji wa juu wa usiku.
"Bundi ni kiashiria cha mazingira yenye afya,Mahali penye bundi mara nyingi huwa na makazi yanayofaa na viumbe wa kutosha,kupotea kwao kunaweza kuashiria uharibifu wa mazingira,"anaeleza
Maganja ameitaja sifa nyingine ya ndege huyo kuwa huchangia utafiti wa kisayansi ambapo Wanasayansi huchunguza mabonge ya mabaki ya chakula (pellets) ya bundi ili kufahamu aina za wanyama waliopo katika eneo, hali ya bioanuwai na mabadiliko ya mazingira.
"Bundi huvutia utalii wa ndege kwa wapenda kutazama ndege (birdwatchers), bundi ni miongoni mwa ndege wanaotafutwa sana hivyo wanaweza kuchangia utalii wa ikolojia na kipato kwa jamii zinazohifadhi mazingira,"amesema n kuongeza;
Ni sehemu ya bioanuwai ambapo kila spishi ya bundi ina nafasi yake katika mtandao wa maisha,kupotea kwake kunaweza kuathiri viumbe wengine wanaomtegemea moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja,"anasema
Anasema,“Bundi husaidia sana kudhibiti panya na wadudu wanaoharibu mazao,bila yeye, wakulima wangeweza kupata hasara kubwa zaidi,” anasema.
Kwa mtazamo huu, bundi si ishara ya mikosi bali ni mshirika wa kimya katika kilimo na usalama wa chakula.
Anaongeza kuwa hakuna ushahidi wa kisayansi unaounganisha sauti ya bundi na matukio ya vifo au misiba ya binadamu. Kila tukio linalotokea baada ya kusikia sauti yake ni mfuatano wa bahati mbaya unaotafsiriwa kimakosa.
“Binadamu hupenda kuunganisha matukio yanayotokea karibu kwa muda, lakini hilo halimaanishi kuna uhusiano wa moja kwa moja,” anasema.
Kwa upande wake Profesa Juma Mkwawa kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) anaeleza kuwa bundi ameumbwa kwa sifa za kipekee zinazomwezesha kuishi usiku kwa ufanisi mkubwa. Macho yake yana uwezo wa kuona kwenye mwanga hafifu, masikio yake husikia harakati ndogo sana, na mbawa zake huruka kimya.
“Haya yote ni marekebisho ya kibiolojia. Si ishara za kiroho wala ujumbe wa mikosi,” anasema.
Profesa Mkwawa anaeleza zaidi kuwa tatizo kubwa ni “ufasiri wa kihisia” wa jamii,tukio la msiba likitokea baada ya mlio wa bundi, binadamu huunganisha matukio hayo mawili kiakili, huku akipuuza mamia ya nyakati ambazo bundi amelia bila tukio lolote baya kutokea.
Hali hii hujenga imani zinazodumu kwa muda mrefu bila msingi wa kisayansi.
Hata hivyo, si sayansi pekee inayoshikilia simulizi hii.
Wazee wa mila wanaona kuwa imani hizi zilikuwa sehemu ya mfumo wa maadili na tahadhari za kijamii.
Mzee Ramadhani Komba wa Kongwa anasema: “Wazee walitufundisha kuwa usiku una mambo yake,hivyo tulijifunza kuheshimu viumbe wa usiku kama sehemu ya maisha ya tahadhari.”
Kwa mtazamo wake, imani hizi hazikuwa za kumhukumu bundi, bali za kuelimisha jamii katika mazingira magumu ya zamani.
"Hivyo Jamii itambue inapomuua bundi kwa hofu na imani potofu, haimuui ndege tu; inamdhoofisha mlinzi wa mazao, msimamizi wa uwiano wa mazingira na kiashiria cha afya ya mfumo wa ikolojia."anasema Mzee Komba
Lakini dunia imebadilika elimu ya mazingira na sayansi ya wanyamapori imeanza kufungua macho ya jamii.
Huu ni ushahidi wa mabadiliko ya polepole ambayo ni muhimu kutoka hofu kwenda uelewa,ni safari ya jamii kutoka katika tafsiri za kiimani kuelekea uelewa wa kisayansi, bila kupoteza kabisa heshima kwa urithi wa kitamaduni.
Nje ya Afrika, hadithi ya bundi ina sura tofauti kabisa,katika Ugiriki ya kale, bundi alihusishwa na hekima na maarifa, akiwa alama ya mungu wa elimu.
Katika baadhi ya maeneo ya Japani, huonekana kama ishara ya bahati njema na ulinzi.
Tofauti hizi zinaonyesha wazi kuwa maana ya bundi si ya asili moja, bali inategemea macho ya anayemtazama.
Hivyo, bundi anabaki kuwa kioo cha jamii yenyewe akionyesha jinsi binadamu tunavyoweza kugeuza kiumbe wa asili kuwa ishara ya hofu au matumaini kulingana na historia na imani zetu.
Lakini ukweli mmoja unabaki thabiti bundi hana uwezo wa kubeba mikosi wala kuleta maafa,anaishi kwa mujibu wa maumbile yake, kimya, usiku, akitimiza jukumu lake katika mfumo mkubwa wa asili.
Mdau wa Mazingira David Mulokozi anaeleza kuwa uhifadhi wa viumbe hai haupaswi kuongozwa na hofu bali na ushahidi wa kisayansi na elimu ya mazingira.
Anasema ni muda wa wanajamii kuafikiana kwamba mapambano ya kweli si dhidi ya bundi, bali dhidi ya upotoshaji unaofanya jamii imuone kama adui na kwamba elimu ya mazingira, tafiti na ushirikiano kati ya taasisi za uhifadhi, viongozi wa jamii na wananchi vinaweza kubadili simulizi hiyo na kujenga kizazi kinachotambua thamani ya kila kiumbe.
"Huenda wakati umefika wa kubadili mtazamo. Badala ya kuendelea kumuona bundi kama ishara ya hofu, jamii inaweza kumtambua kama sehemu ya urithi wa asili unaostahili kulindwa,kwa kufanya hivyo, si bundi pekee atakayekuwa salama, bali pia mfumo wa ikolojia ambao maisha ya binadamu yanategemea,"anaeleza.
Kama kuna somo la kubeba kutoka kwenye simulizi hii, basi ni hili; bundi hakuwahi kuwa tatizo… bali tulihitaji muda tu wa kumuelewa.
Huenda kwa muda mrefu bundi ameishi kama kiumbe asiye na mtetezi, akibeba mizigo ya hofu za binadamu bila nafasi ya kusikilizwa.
Amehukumiwa kimya kimya, akihusishwa na mikosi na ishara zisizo na ushahidi, huku ukweli wake ukifunikwa na pazia la imani za muda mrefu.
Na huenda leo, bundi amepata mtetezi wake. Siyo kwa sababu amebadilika, bali kwa sababu Kuna Mtetezi anayesema wazi kuwa nyuma ya hofu zote hizo, kuna kiumbe asiye na kosa kiumbe anayefanya kazi yake ya asili kwa utulivu wa usiku, bila kujua kuwa amebebeshwa maana ambazo si zake.
Mimi, katika safari hii ya kuandika na kuchunguza, naamini nimeanza kuwa si tu mwandishi wa hadithi ya bundi, bali mtetezi wake. Na huenda jamii ikatambua siku moja kwamba sauti hii ndogo ya utetezi ilikuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa. Kwa sababu ukweli unabaki mmoja: bundi hakuhitaji hofu yetu alihitaji tu mtu wa kumuelewa.
Ninaamini kwamba siku moja sauti ya bundi usiku haitasikika tena kama ishara ya hofu, bali kama ukumbusho kwamba mazingira bado yanaishi na kwamba binadamu ana wajibu wa kulinda kila kiumbe anayeshirikiana nacho katika sayari hii.
Mapambano ya kweli hayapaswi kuwa dhidi ya bundi, bali dhidi ya imani potofu zinazochochea uharibifu wa viumbe hai. Elimu ya mazingira, tafiti na ushirikiano kati ya wataalamu, viongozi wa jamii na wananchi vinaweza kubadili mtazamo huo na kuifanya jamii itambue kuwa kila kiumbe kina nafasi yake katika uhai wa dunia.




Social Plugin