
Na Amina Saidi, Tanga
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, amesisitiza umuhimu wa vijana kufundishwa historia na misingi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili waweze kukielewa na kukilinda chama hicho kwa vizazi vijavyo.
Akizungumza kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 49 ya CCM, Abdullah alisema kuwa uelewa wa historia ya chama hicho utawasaidia vijana kuenzi misingi yake na kuendeleza maono yaliyoasisiwa na waasisi wake.
Kiongozi huyo, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na mlezi wa chama mkoa wa Tanga, alitoa wito huo wakati wa kilele cha maadhimisho ya kuzaliwa kwa CCM ngazi ya mkoa. Maadhimisho hayo yalifanyika katika viwanja vya stendi ya Bombani, wilayani Muheza, ambapo viongozi na wanachama mbalimbali walikusanyika kuadhimisha safari ya chama hicho tangu kuanzishwa kwake.
Alisema ni muhimu kwa vijana kufahamu misingi ya kuanzishwa kwa CCM, ikiwemo sababu za kuungana kwa vyama vya TANU na ASP, kwani bila uelewa huo kuna sehemu muhimu ya historia ya taifa watakuwa wanaikosa.
Aidha, Abdulla aliwataka wananchi kumpa ushirikiano Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake cha uongozi, akieleza kuwa ameahidi na kuanza kutekeleza mambo mengi yenye manufaa kwa taifa.
Aliongeza kuwa CCM ni chama pekee kinacholinda na kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, huku akidai kuwa baadhi ya vyama vya siasa vinazungumzia kuvunja Muungano huo wakati wa kampeni, jambo alilosema si lenye afya kwa ustawi na maendeleo ya nchi.
Akizungumzia maendeleo ya mkoa wa Tanga, Abdullah alisema serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 429 katika upanuzi wa Bandari ya Tanga chini ya uongozi wa Rais Samia. Pia alitaja maombi ya ujenzi wa uwanja wa ndege mkoani humo ambayo serikali imeanza kuyafanyia kazi.
Vilevile, alieleza kuwa ujenzi wa miradi mbalimbali ya miundombinu unaendelea, ikiwemo barabara ya Handeni–Kibirashi–Kipindi inayounganisha na mkoa wa Singida, pamoja na barabara nyingine muhimu zinazolenga kuimarisha usafirishaji na kukuza uchumi kwa kuunganisha mikoa na Bandari ya Tanga.

Social Plugin