Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kimeendelea kutoa wahitimu mahiri wenye ujuzi wa kitaaluma, maadili na uwezo wa kiuongozi, wenye uwezo wa kuleta mabadiliko chanya katika taasisi na jamii wanazozihudumia.
Akizungumza Februari 6, 2026, wakati wa mahafali ya 27 ya wahitimu wa Shahada ya Uzamili ya mwaka 2025 yaliyofanyika katika Ukumbi wa Ngurdoto mkoani Arusha, Mkuu wa Chuo Profesa Eliamani Sedoyeka, amesema maboresho yanayoendelea katika huduma za ufundishaji na ujifunzaji yameiwezesha IAA kuandaa wataalamu wanaokidhi mahitaji ya taifa na soko la ajira.
Prof. Sedoyeka amewasisitiza wahitimu kuzingatia misingi ya uwajibikaji, uadilifu na uzalendo wanapotekeleza majukumu yao huku akiwataka kutumia ujuzi wa kisayansi, tafiti na maadili katika kufanya maamuzi katika maeneo watakayoaminiwa kuyahudumia.
“Mmeandaliwa kuwa viongozi wenye maarifa, maadili na uwezo wa kuongoza mabadiliko chanya katika taasisi na jamii mnazozihudumia, Ni wajibu wenu kuzingatia uwajibikaji, uadilifu na uzalendo katika kila jukumu mtakalotekeleza,” amesema Prof. Sedoyeka.
Akizungumzia mchango wa tafiti zilizofanywa na wahitimu, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo, Dkt. Mwamini Tulli, amesema tafiti hizo ni msingi muhimu katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, kuboresha utoaji wa huduma na kuchochea ukuaji wa uchumi endelevu.
Dkt. Tulli amesisitiza kuwa matokeo ya tafiti zilizofanywa na wahitimu hazipaswi kubaki kwenye makabati bali yatumike kutatua changamoto halisi zinazolikabili taifa na taasisi zake.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula, ameupongeza uongozi wa IAA kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya kisasa inayoendana na mabadiliko ya teknolojia duniani, hali iliyowawezesha kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Naibu Waziri amethibitisha kuwa hatua hiyo ni ishara ya dhamira ya huo katika kuhakikisha mifumo ya ufundishaji na ujifunzaji inaendana na mahitaji ya dunia ya sasa na ya baadaye.





Social Plugin