Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UMIKIDO WAPEWA BARAKA NA TCRA



Na mwandishi wetu, Dodoma

Viongozi wa Umoja wa Vyombo vya Habari vya Mitandao ya Kijamii Mkoa wa Dodoma (UMIKIDO) wakiongozwa na Mwenyekiti Ben Majata, wamefanya ziara ya kujitambulisha katika Ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) – Kanda ya Kati zilizopo jijini Dodoma.

Katika ziara hiyo, iliyofanyika leo Februari 9, 2026 viongozi wa UMIKIDO walifanya mazungumzo na Meneja wa TCRA Kanda ya Kati Mhandisi Asajile John na kueleza malengo ya kuanzishwa kwa umoja huo pamoja na dira ya kukuza taaluma na uendeshaji wa vyombo vya habari vya mitandao ya kijamii kwa kuzingatia sheria na maadili ya uandishi.

Kwa upande wake, Meneja wa TCRA Kanda ya Kati, Mhandisi John, ameukaribisha UMIKIDO kwa ushirikiano wa karibu, ikiwemo kuandaa mafunzo kwa wanachama na kuwahimiza kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, sambamba na kusajili vyombo vyao na kupata leseni rasmi kutoka mamlakani.

Aidha, ameeleza kuwa maboresho mbalimbali yanayoendelea kufanywa na TCRA yanalenga kupunguza malalamiko ya waendeshaji wa vyombo vya habari mitandaoni na kuboresha mazingira ya kazi katika sekta hiyo.

Pia amewahimiza kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali ili kujiimarisha kitaaluma na kiuchumi.

Viongozi wengine walioshiriki ziara hiyo ni Emmanuel Charles (Katibu wa UMIKIDO), Zena Chitwanga (Mhasibu), Daniel Mkate (Afisa Mahusiano), Alex Sonna (Kiongozi wa Kamati ya Ufuatiliaji), Henry Masanja (Kiongozi wa Kamati ya Nidhamu) na Ronald Sonyo (Kiongozi wa Kamati ya Fedha na Mipango).


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com