Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KWAGILWA AAGIZA HATUA ZA KINIDHAMU KWA MTENDAJI WA KATA KIPUNGUNI B



Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Reuben Kwagilwa (Mb) amemwelekeza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya Mtendaji wa Kata ya Kipunguni ‘B’ kwa kuchelewa kufika kazini na kushindwa kutoa huduma kwa wananchi ipasavyo.


Mhe. Kwagilwa ametoa maelekezo hayo leo tarehe 09 Februari,2026  mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za kata hiyo majira ya saa 1:40 asubuhi na kukuta ofisi ikiwa imefungwa, hali aliyosema ni kinyume na kanuni za utumishi wa umma.


Akizungumza baada ya kufika Ofisinih apo, Mhe. Kwagilwa amesema kufungwa kwa ofisi wakati wa kazi kunakwamisha juhudi za Serikali katika kuwahudumia wananchi.


“Serikali imeajiri watu ili iwahudumie wananchi. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka Watanzania wasikilizwe, wahudumiwe na watatuliwe kero zao. Hatutafikia malengo hayo kama ofisi ya umma inakuwa imefungwa namna hii.” Amesema Mhe. Reuben Kwagilwa


Aidha, Mhe. Kwagilwa amemtaka mtendaji huyo ambaye hakuwapo eneo la kazi, kuripoti kwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam na kutoa maelezo ya kwanini ofisi ya umma ilikuwa imefungwa wakati wa saa za kazi.


Kanuni F.1 ya kanuni za kudumu za Utumishi wa Umma za mwaka 2009 inamtaka mtumishi wa Umma kuripoti kazini saa 1.30 na kutekeleza majukumu yake hadi saa 9.30 alasiri.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com