Umoja wa Kikundi Kazi cha Asasi za Kiraia zinazopambana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani Shinyanga (SHYEVAWC) wakipatiwa mafunzo ya uponyaji wa kihisia na kisaikolojia kutoka kwa mwezeshaji Dk. Katanta Simwanza.
Na Estomine Henry na Stella Herman,Shinyanga
Umoja wa Kikundi Kazi cha Asasi za Kiraia zinazopambana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani Shinyanga (SHYEVAWC) umeendesha mafunzo ya uponyaji wa kihisia na kisaikolojia kwa wanachama wake kutoka asasi za kiraia zipatazo 35, yakilenga kuimarisha ustawi wa afya ya akili na ufanisi wa utendaji kazi.
Akifungua mafunzo hayo leo, Februari 6, 2026, mjini Shinyanga, Mwenyekiti wa SHYEVAWC, Jonathan Manyama, alisema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwasaidia wanachama kuponya athari za kihisia na kisaikolojia zilizotokana na changamoto za kifamilia, kitaasisi na kijamii walizokumbana nazo mwaka 2025.
Manyama amesema kuwa wanachama wa asasi za kiraia wanabeba majukumu mazito ya kuhudumia jamii, hivyo ni muhimu wawe na uimara wa kisaikolojia na kihisia ili kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
“Majukumu yetu ya kila siku ni kusaidia jamii, hivyo ni lazima tujiandae vizuri kisaikolojia na kihisia. Wanachama wetu ni rasilimali muhimu, na wanapaswa kuwa na nguvu mpya, uwajibikaji na ufanisi utakaotokana na mafunzo haya,” alisema Manyama.
Amesisitiza pia umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa wanachama wa SHYEVAWC, akibainisha kuwa kutambua na kuheshimu vipawa vya kila mmoja kunasaidia kufanya maamuzi makubwa na mipango yenye tija kwa ajili ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
“Katika dunia ya sasa, maendeleo yanategemea mshikamano na kufanya kazi kwa pamoja bila kujitenga. Hii hutusaidia kutatua changamoto za kifamilia na kitaasisi kwa pamoja,” aliongeza.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mchungaji Meshaki Kulwa, ambaye alikuwa mwezeshaji, alisema kuwa hazina kubwa ya maisha ya mwanadamu ni uwezo wa kuhusiana na jamii (social network), jambo linalosaidia kujenga maendeleo endelevu.
“Kujenga mfumo wa ushirikiano wa mara kwa mara kunamwezesha kila mtu kutambua karama na talanta za mwenzake na kuzitumia kwa pamoja kwa ustawi wa jamii,” alisema Mchungaji Kulwa.
Ameongeza kuwa jamii inapaswa kuondokana na tabia ya kuficha changamoto za kihisia na msongo wa mawazo, akisisitiza kuwa kusema na kushirikiana na watu sahihi ni hatua muhimu ya uponyaji wa afya ya akili.
“Changamoto kubwa katika jamii yetu ni kuwaambia watu wasiseme wanachopitia. Msingi wa uponyaji ni kusema na kupata ushauri wa kitaalamu ili kulinda afya ya akili,” alifafanua.
HYEVAWC kutoka shirika la COED, pamoja na Annascolastika Ndagiwe wa Shirika la Wanawake Laki Moja, walisema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wanachama wao na kwa jamii kwa ujumla.
Wameeleza kuwa maarifa waliyoyapata yatawawezesha kushughulikia changamoto za kihisia na kisaikolojia wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu ya kijamii.
Social Plugin