
Na Bora Mustafa,Arusha.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla, ameipongeza Menejimenti na wafanyakazi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) kwa mchango wao mkubwa katika kukuza utalii wa mikutano pamoja na kulitangaza taifa kimataifa.
Makalla ametoa pongezi hizo Februari 6, 2026, wakati wa kikao cha kawaida cha Baraza la Wafanyakazi wa AICC, akisema kituo hicho kimefanikiwa kuratibu mkutano wa kimataifa ulioshirikisha nchi zaidi ya 120 uliofanyika hivi karibuni jijini Arusha.
Pia amesema mafanikio hayo yanaonesha wazi kuwa AICC imejipanga kikamilifu kuhudumia Mkutano wa Bunge la Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu jijini Arusha.
Aidha Makalla amesema AICC imekuwa na mchango mkubwa katika kuutangaza Mkoa wa Arusha na Tanzania kwa ujumla katika ramani ya kimataifa, akiwataka wafanyakazi wote wa kituo hicho kuwajibika ipasavyo katika kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maono na malengo ya Serikali.
Amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha utoaji wa huduma ikiwemo huduma za ukarimu na itifaki, pamoja na kuongeza matumizi ya teknolojia ya kisasa ili kuvutia zaidi mikutano ya kimataifa kufanyika katika kituo hicho.
Amesema AICC inapaswa pia kujiandaa kikamilifu kutumia fursa zitakazotokana na Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), ambapo baadhi ya michezo itachezwa jijini Arusha.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa AICC, Bi. Christine Mwakatobe, amesema kituo hicho kwa sasa kimepata ithibati ya kimataifa katika sekta ya mikutano duniani.
Amesema mpango wa AICC ni kuendelea kuboresha utoaji wa huduma pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia ili kuongeza ushindani katika soko la kimataifa la mikutano.
Pia Mwakatobe amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema jitihada zake katika kukuza diplomasia, mahusiano ya kimataifa pamoja na kuimarisha amani na utulivu nchini zimeiwezesha AICC kupata fursa zaidi za kimataifa.




Social Plugin