
Na OWM- TAMISEMI, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM- TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe ameridhishwa na hatua iliyofikiwa ya maandalizi ya ufunguzi Soko Kuu la Kariakoo lililopo Ilala Jijini Dar es Salaam.
Prof. Shemdoe ameyasema hayo leo Februari 07, 2026 alipotembelea soko hilo ili kujiridhisha na maandalizi ya hafla ya ufunguzi wa soko hilo litakalofunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Kesho Februari 08, 2026.
Prof. Shemdoe amemshukuru Mhe. Rais kwa uwekezaji uliofanyika katika soko hilo lililoungua mwaka 2021 ambalo limefanyiwa ukarabati na kujengwa soko lingine jipya lenye ghorofa sita (6) katika eneo hilo.
"Ninamshukuru Mhe. Rais kwa Shilingi Bilioni 28 aliyoridhia itumike kwa ajili ya ukarabati na ujenzi huu, hii ni hatua kubwa sana ambayo tunapaswa kujivunia," amefafanua Prof. Shemdoe.
Soko Kuu la Kariakoo liliungua Julai 10, 2021 na Mhe Rais alipotembelea soko hilo kuwapa pole wafanyabiashara waliopatwa na kadhia hiyo, aliahidi kuwa atafanya ukarabati na kuliboresha zaidi, ahadi ambayo ameitekeleza kwa vitendo.
Prof .Shemdoe amewasihi wananchi na wafanyabiashara wa Jiji la Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi wa soko hilo huku akiwapongeza viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam, Jiji la Dar es Salaam pamoja na uongozi wa Shirika la Masoko ya Kariakoo kwa namna walivyoshirikiana na kufanikisha maandalizi hayo kwa kiwango cha juu.
Katika ziara hiyo Prof. Shemdoe ameambatana na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, Bw. Adolf Ndunguru, Naibu Katibu Mkuu-TAMISEMI, Bw. Sospeter Mtwale, Katibu Tawala, Bw. Abdul Mhinte, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Bw. Elihuruma Mabehe na viongozi waandamizi wa Wizara hiyo.






Social Plugin