
Na OWM - TAMISEMI, Muheza
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, Kwa mujibu wa Kanuni ya 37(1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022, amemuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza akisimamiwa na RAS kuwapumzisha kutekeleza majukumu yao watumishi 14 wa Halmashauri hiyo ambao wanatuhumiwa kusababisha changamoto zilizokwamisha ujenzi wa jengo la utawala.
Prof. Shemdoe amewataja watumishi hao wanaosimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi ni Afisa Hesabu Mwandamizi Rajabu Diamond Mushi, Mhandisi wa Kilimo Mkuu Abdallah Mohamed Jaha, Afisa Ugavi Msaidizi Shukuru Elias Marandu, Afisa Rasilimaliwatu Jesca Francis Luvigo, Mhandisi Careen Dustan Meela, Mkuu wa Idara ya Manunuzi Mwangaza Rajabu Kusenge, Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi Pilly Maximilian Sindanguru na Kaimu Mkuu wa Idara ya Huduma za Sheria Angela Jabe Mwapachu.
Amewataja wengine kuwa, ni Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Edward Sempindu Mgaya, Mkuu wa Kitengo cha Michezo, Utamaduni na Sanaa Msafiri Charles Nyaluva, Mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi Zautuni Said Abdallah, Mkuu wa Kitengo cha Uhifadhi wa Mazingira Issa Selemani Msumari, Mhasibu Nasibu Fadhili Mashanjala na Mhasibu Moses Herbert Mpembo.
Prof. Shemdoe amefafanua kuwa, yeye pamoja Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete walipeleka wataalam kutoka pande zote mbili, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Mkuu, ambaye wakati wa ziara yake ya kukagua mradi wa jengo la utawala Muheza alibaini uwepo wa changamoto katika utekelezaji wa mradi huo na kuelekeza wachukue hatua za haraka kubaini wahusika na kuwachukulia hatua stahiki.
Prof. Shemdoe amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, kwa mujibu Kanuni ya 36 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022 kuunda Kamati ya Uchunguzi wa Awali ili kuwachunguza watumishi hao 14 wanaotumiwa kukwamisha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo la utawala. Amemuelekeza pia RAS kufuatilia na kumsimamia DED kupata timu ya watu waadilifu watakaokuwa kwenye kamati hiyo ili kufanya uchunguzi wa suala hilo.
Pia, amemtaka mkurugenzi huyo, kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi waliotajwa na ambao hawakutajwa endapo watabainika kuhusika katika kusababisha changamoto katika utekelezaji wa mradi huo baada ya uchunguzi wa awali kukamilika.
Aidha, kwa wahusika waliotajwa katika taarifa za awali wasio watumishi Umma, Prof. Shemdoe amevielekeza vyombo vinavyohusika na uchunguzi ikiwemo Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchukua hatua stahiki dhidi yao.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema, majukumu ya ofisi yake pamoja na ya Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI ni kuratibu masuala ya utumishi wa umma nchini, kwani Ofisi ya Rais UTUMISHI ndio mwajiri mkuu anayewapangia watumishi vituo vya kazi na vituo hivyo vinasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI.
Mhe. Kikwete ameongeza kuwa, linapotokea jambo linalohusu masuala ya kiutumishi yeye Waziri wa UTUMISHI na Waziri wa TAMISEMI wanahusika kusimamia na kuratibu utekelezaji wa majukumu ya watumishi wa umma na ndio maana Mhe. Waziri Mkuu Dkt. Nchemba amewaelekeza kushugulikia changamoto hiyo ya utekelezaji wa Mradi wa jengo hilo.
Maelekezo aliyoyatoa Mhe. Waziri Mkuu kwa mawaziri hao, yalitokana na kubaini uwepo wa changamoto ya upotevu wa nondo 700 zenye thamani ya Shilingi 9,200,000.00 zilizonunuliwa kutoka Saifi Store, upotevu wa marine board 192 zenye thamani ya Shilingi 7,800,000.00, upotevu wa mifuko ya saruji 300 yenye thamani ya shilingi 4,400,000.00, kufanyika malipo ya kiasi cha Shilingi 110,600,000.00 kwa mhandisi mshauri Edge Engineering and Consulting Limited bila uwepo wa Mkataba na Shilingi 343,900,000.00 kutumika nje ya mradi kwa kulipana posho.






Social Plugin