Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

POLISI MBEYA WAFICHUA UKWELI WA MAUAJI YA MWENYEKITI WA CCM ITUMBI


Na mwandishi wetu, Mbeya

Kupitia mitandao ya kijamii kunasambazwa picha mjongeo akionekana mtu mmoja mwanaume ambaye anajinasibu kuhusika katika tukio la mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Tawi la Itumbi aitwaye Elia Richard Sambala, miaka 53, mkazi wa Itumbi Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya.

Ukweli ni kwamba, Februari 11,2026 saa 7 mchana katika Kijiji cha Itumbi, Elia Richard Sambala, alikutwa shambani kwake akiwa amejeruhiwa kwa kukatwa na kitu chenye makali kichwani na watu wasiojulikana na alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa Hospitali ya Wilaya ya Chunya kwa matibabu.

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, kupitia Askari wa kuchunguza matukio ya mauaji, walianza msako mkali na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili kuhusiana na tukio hilo na ufuatiliaji zaidi kwa wengine waliohusika unaendelea.

Uchunguzi wa awali umebaini kuwa, chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa masilahi wa eneo la uchimbaji madini ya dhahabu ambapo mmoja wa wanafamilia hao alikodisha kwa wawekezaji raia wa China kwa ajili ya shughuli za uchimbaji bila kushirikisha ndugu wengine.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa onyo kali kwa mtu huyo anayejinasibu kuwa ni kiongozi wa kikosi anachokiita TFF [Tanzania Freedom Fighters] kuacha kuongelea jambo ambalo ni tofauti na uhalisia na kuacha kutumia vibaya mitandao ya kijamii kupotosha ukweli na kuhamasisha uhalifu dhidi ya Taasisi, Viongozi na Wananchi. Upelelezi unaendelea na jitihada za kumtafuta mtu huyo ili kumkamata kwa hatua za kisheria zinaendelea.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com