Na Mwandishi Wetu
KATIKA kupunguza migogoro ya mirathi katika jamii ya Watanzania Shirika la MIRATHI TANZANIA (MITA) imezindua programu ya utoaji elimu ya mirathi mashuleni huku jamii ikielezwa kuwa somo la mirathi sio kifo bali kuandika mirathi mapema sio kujichulia kifo bali ni somo la maisha na ustawi wa waliobaki.
Uzinduzi wa Programu ya utoaji elimu ya mirathi mashuleni yenye kauli mbiu inayosema “Mirathi ni Amana; Linda Haki ya Mjane na Yatima imezinduliwa leo Februari 3,2026 katika Shule ya Sekondari Nguva iliyopo Kigamboni mkoani Dar es Salaam .
Akizungumza kwa niaba Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam Dalmia Mikaya,Ofisa Tarafa Wilaya ya Kigamboni Agusta Safari amesema wanalipongeza Shirika la MITA kwa kuja na programu hiyo ya utoaji wa elimu ya mirathi mashuleni kwani moja ya changamoto iliyopo katika jamii ni uwepo wa migogoro inayotokana na mirathi katika familia.
“Hili ni wazo la kimapinduzi kwa sababu mnaanza kujenga msingi wa uelewa wa kisheria kwa vijana wetu wakiwa bado wadogo.Nawaasa wanafunzi wote wasikilize kwa makini elimu hii na kusomaJarida maalumu ambalo litagawanywa bure kwa wanafunzi.
Kuhusu mantiki ya elimu ya mirathi kwa wa kwa Wanafunzi amesema imekuwa ikishuhudiwa mara nyingi familia zikisambaratikamara baada ya mzazi au mlezi kufariki dunia. Migogoro ya mirathi imekuwa chanzo kikubwa cha wanafunzi kuacha shule kwa kukosaada na mahitaji, watoto kufukuzwa kwenye nyumba walizozaliwakutokana na dhuluma.
Pamoja na hayo amesema Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejikita katika kusimamia haki za wanyonge, hususan wanawakena watoto. “Kampeni hii ni sehemu ya jitihada hizo za kuhakikisha hakuna mtoto anayekatishiwa ndoto zake kwa sababu ya dhuluma ya mali.”
Kwa upande wake Katibu Mkuu Mtendaji wa MITA amesema Rose Fusi amesema programu hiyo ya utoaji elimu ya mirathi mashuleni inalenga kuwapa vijana uelewa wa kisheria na kimaadili kuhusu usimamizi wa mali za marehemu na haki za warithi mapema kabla hawajakumbana na changamoto hizo katika maisha ya utu uzima.
“Taasisi ya MIRATHI TANZANIA (MITA) tunamshukuru Balozi wa Ireland hapa nchini, MS. Nicola Brennan, kwa kutoa ufadhili wa programu hii ya kutoa elimu ya mitathi mashuleni kwani ufadhili wake ni mbegu njema iliyopandwa kwenye ardhi ya Kigamboni ambayo itaota na kuzaa matunda mema kwa ustawi wa Taifa zima. “
Akifafanua zaidi amesema programu hiyo pia inalenga kujenga uelewa huo ili kuweka kinga dhidi ya dhuluma na migogoro ya kifamilia kwa kuwa watoto watakuwa mabalozi wa haki na kuwa chachu ya mabadiliko chanya ya fikra kwa wazazi na walezi na kuchochea uandishi wa wosia.
Akifafanua zaidi amesema kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, wanalenga kuwa na jamii yenye utawala wa sheria na usawa wa kijamii na kiuchumi. “Kwa kuwa Dira ya 2050 inategemea pakubwa katika uwekezaji, bila elimu ya mirathi,uwekezaji wa wazazi hupotea mikononi mwa warithi wasio na uelewa au kupitia dhuluma.
Wakati huo huo Cainess Samweli ambaye ni Ofisa Ustawi was Jamii Wilaya ya Kigamboni amesema kuwa elimu hiyo ambayo imezinduliwa mashuleni itakwenda kuamsha uelewa kwa jamii na hivyo kuepusha migogoro inayotokana na mirathi iliyoachwa katika familia.
Kwa upande wao wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nguva wamesema kutolewa kwa elimu ya mirathi mashuleni wanaamini wanafunzi wengi watakuwa na uelewa huku wakieleza kuna baadhi ya wanafunzi wamekatisha masomo kutokana na migororo ya mirathi ambayo imejitokeza katika familia zao.






















Social Plugin