Mbunge wa Jimbo la Mtumba Mkoani Dodoma, Mhe. Anthony Mavunde, ambaye pia ni Waziri wa Madini amezindua kisima cha maji katika Mtaa wa Msalato, Ubalozi wa Catherine Mwajoka, kwa ajili ya matumizi ya wananchi.
Uzinduzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi aliyoitoa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kuhusu kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa eneo hilo.
Akizungumza na wananchi mara baada ya uzinduzi huo, Mheshimiwa Mavunde amewataka wakazi wa Msalato kulinda na kutunza miundombinu ya kisima hicho ili kiweze kudumu na kuwanufaisha kwa muda mrefu.
Amesisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.
Aidha, ameahidi kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ya Msalato na Jimbo la Mtumba kwa ujumla, kwa kushirikiana na viongozi wengine wa Serikali.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Mavunde amewashukuru wananchi wa Msalato kwa imani kubwa waliyoionesha kwa kumpigia kura Samia Suluhu Hassan, yeye kama Mbunge pamoja na Diwani wao wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2025, akieleza kuwa ushindi huo unampa nguvu ya kuendelea kuwatumikia wananchi kwa bidii na uadilifu.















Social Plugin