Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAMLAKA YA RUFANI YAIMARISHA HAKI ZA WAZABUNI KUPITIA MFUMO WA KIDIJITALI NeST



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Katika kuimarisha uwazi na upatikanaji wa haki kwenye ununuzi wa umma, Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imeendelea kufanya mageuzi ya kidijitali kwa kuimarisha matumizi ya mfumo wa NeST unaowezesha wazabuni kuwasilisha malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 25, 2026 jijini Dodoma, Katibu Mkuu Mtendaji wa Mamlaka hiyo, James Sando, amesema mfumo huo umeunganisha taasisi zote nunuzi nchini, hatua inayomruhusu mzabuni kuwasilisha rufaa yake kwa haraka, kwa uwazi na bila urasimu.

Amesema kupitia mfumo huo, Mamlaka ina uwezo wa kufuatilia nyaraka zote zinazohusiana na zabuni inayolalamikiwa, jambo linalosaidia kufanya maamuzi yenye haki kwa kuzingatia vielelezo halisi.

Katika kuhakikisha mfumo huo unatumika ipasavyo, Sando amesema Mamlaka imekuwa ikitoa mafunzo ya matumizi ya moduli ya malalamiko na rufaa kwa wadau wa ununuzi wa umma, hususan vijana na makundi maalum, ili kuwajengea uelewa wa taratibu za kudai haki zao kwa mujibu wa sheria.
Ametoa wito kwa wazabuni na wadau wote wa ununuzi wa umma kujitokeza kushiriki mafunzo hayo pindi yanapotangazwa, akieleza kuwa uelewa wa matumizi sahihi ya mfumo ni msingi wa ufanisi wake.

Hatua nyingine kubwa inayotarajiwa, kwa mujibu wa Sando, ni mpango wa kuiunganisha moduli ya malalamiko na rufaa ya NeST na mfumo wa Mahakama katika mwaka wa fedha ujao, jambo litakalorahisisha zaidi mchakato wa haki na kuongeza imani ya wazabuni katika mifumo ya ununuzi wa umma.

Mageuzi hayo yanaelezwa kuwa sehemu ya juhudi za Serikali katika kujenga mazingira yenye uwazi, ushindani wa haki na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com