
Na Bora Mustafa, Arusha
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mhe. Paul Christian Makonda, amefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo jijini Arusha, akisisitiza ubora wa kazi na kukamilika kwa miradi hiyo kwa wakati.
Katika ziara hiyo aliyofanya leo Februari 3,2026 Waziri Makonda ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Amos Makalla , Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Joseph Modest Mkude, pamoja na viongozi wengine wa jiji la Arusha na Mkoa wa Arusha.
Miongoni mwa miradi aliyotembelea kwa kipaumbele ni pamoja na ujenzi wa Stendi ya Mabasi ya Bondeni City, ambapo Waziri Makonda amepata fursa ya kujionea maendeleo ya ujenzi huo na kuzungumza na wakandarasi pamoja na wasimamizi wa mradi.
Akizungumza katika eneo la mradi huo, Mhe. Makonda ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Arusha kwa usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo, akieleza kuwa ufuatiliaji wa karibu wa viongozi katika maeneo ya miradi ni nguzo muhimu ya kuhakikisha thamani ya fedha za umma inaonekana.
Amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuhakikisha stendi hiyo inakamilika kwa wakati uliopangwa na kwa kuzingatia viwango vya juu vya ubora, ili iweze kutoa huduma bora, salama na ya kisasa kwa wananchi pamoja na wageni wa Jiji la Arusha.
Aidha, Waziri Makonda ameuagiza uongozi wa mkoa kushirikiana kwa karibu na wataalamu wa mipango miji ili kutumia kikamilifu fursa za kiuchumi zitakazotokana na uwepo wa stendi hiyo, ikiwemo kuanzisha maeneo ya biashara na huduma mbalimbali yatakayochochea ajira na kukuza uchumi wa jiji.
Katika hatua nyingine, Mhe. Makonda amewakumbusha wananchi wa Arusha umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari, akisisitiza kuwa mapato ya ndani ndiyo msingi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na chachu ya kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.










Social Plugin