Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAGEUZI MAKUBWA SEKTA YA KILIMO YATARAJIWA KANDA YA KASKAZINI


Na Bora Mustafa, Arusha.

Mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo, ufugaji na masoko yanatarajiwa kufanyika baada ya wadau wa sekta hiyo pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali za mikoa ya Kanda ya Kaskazini kukutana jijini Arusha kujadili mikakati ya kumnyanyua mkulima mdogo, kutafuta masoko ya uhakika pamoja na kujenga maghala ya kisasa ili kuzuia upotevu wa mazao baada ya mavuno.

Akizungumza katika mkutano huo ,Februari 10,2026 Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burhani, amesema serikali itaendelea kuhakikisha uhamasishaji, ukuzaji na uendelezaji wa shoroba za kilimo kwa lengo la kuongeza tija na ushindani wa mazao ya wakulima. Amesema kipindi kijacho nchi inatarajia kupokea wageni wengi, hivyo ni wakati muafaka kwa wadau wa kilimo kujipanga vizuri ili kunufaika na fursa zilizopo.

Aidha, Balozi Burhani amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wanawake na vijana kwa upana katika shughuli za kilimo, huku akiwashauri kujikita katika kilimo chenye soko, ikiwemo kilimo cha mbogamboga na matunda.

Amesema sekta ya kilimo ni sekta mtambuka inayogusa sekta nyingine nyingi ikiwemo biashara, viwanda na ardhi. Hata hivyo, amebainisha kuwa sekta hiyo pia ni chanzo kikubwa cha ajira kwa Watanzania wengi.

 “Nawaomba wataalamu wa AGCOT na ATO kusambaza uzoefu wenu kwa wadau wote wa kilimo ili kufikia malengo yaliyowekwa ifikapo mwaka 2030,” amesema Balozi Burhani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Agriculture Transformation Office (ATO), Elizabeth Missokia, amesema lengo la mkakati huo ni kuwaunganisha wakulima na masoko ya ndani na nje ya nchi, kuimarisha sekta binafsi, pamoja na kuweka mfumo madhubuti wa tathmini na ufuatiliaji wa uzalishaji. Amesema mkakati huo pia unalenga kuhamasisha kilimo cha mazao ya kusindika ili kuongeza thamani ya mazao.

“Katika mageuzi haya tutazingatia ujumuishi wa wanawake na vijana. Pia, kwa takribani miaka kumi tumekuwa na shoroba moja ya kilimo ambayo imechangia mageuzi ya uzalishaji wa chakula kwa zaidi ya asilimia 65,” amesema Missokia.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, amesema mageuzi hayo yakitekelezwa kikamilifu yatachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza umaskini kwa wakulima wadogo nchini.

Amesema kwa muda mrefu wakulima wamekuwa wakishuhudia mazao yao yakiozea mashambani kutokana na kukosekana kwa masoko ya uhakika.

 “Naamni huu utakuwa mwarobaini kwa wakulima wadogo ambao ndio wenye idadi kubwa nchini,” amefafanua Mkude.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com