Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAFUNZO YA MLM KUIMARISHA USHIRIKIANO NA UFANISI KATIKA HUDUMA ZA CHANJO


Mafunzo ya Wasimamizi wa Ngazi ya Kati (Mid-Level Managers – MLM) yana mchango mkubwa katika kuimarisha ushirikiano, uratibu na uwezo wa usimamizi wa huduma za chanjo kuanzia ngazi ya mkoa hadi halmashauri.


 Kupitia mafunzo haya, viongozi wa ngazi ya kati huwezeshwa kuboresha mipango, kufanya maamuzi yenye tija, kusimamia rasilimali kwa ufanisi na kuhakikisha huduma za chanjo zinawafikia wananchi wote bila ubaguzi, hususan watoto na makundi yaliyo katika hatari zaidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yanayofanyika mkoani Tabora kuanzia tarehe 9 hadi 13 Februari, 2026, Mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Bi. Linda Chatilla, amesema Serikali inaendelea kuweka mkazo katika kujenga uwezo wa wasimamizi wa ngazi ya kati kwa kuwa wao ndio kiungo muhimu kati ya sera za kitaifa na utekelezaji wa huduma za afya katika jamii.


Amebainisha kuwa ushirikiano wa karibu baina ya mikoa na halmashauri ni msingi wa mafanikio ya programu za chanjo pamoja na huduma nyingine za afya, huku akisisitiza umuhimu wa mshikamano, uwajibikaji na uratibu wa pamoja katika kufikia malengo ya sekta ya afya.


Bi. Chatilla ameongeza kuwa mafunzo ya MLM yanalenga kuimarisha mifumo ya uwajibikaji, ufuatiliaji na tathmini ya huduma za chanjo, pamoja na kuboresha matumizi ya takwimu katika kupanga na kufanya maamuzi sahihi, hatua itakayosaidia kuongeza wigo wa chanjo na kudhibiti milipuko ya magonjwa yanayoweza kuzuilika.


Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Honoratha Rutanisibwa, ameeleza kuwa chanjo ni mojawapo ya afua muhimu zaidi za afya ya umma zilizoleta mafanikio makubwa katika kupunguza vifo, ulemavu na magonjwa hatarishi, hasa kwa watoto wachanga na akina mama. Amesisitiza kuwa huduma bora za chanjo husaidia kulinda afya ya jamii kwa ujumla, kupunguza mzigo wa magonjwa na gharama za matibabu kwa familia na taifa.


Dkt. Rutanisibwa amefafanua kuwa mafanikio ya programu za chanjo yanategemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa wasimamizi wa ngazi ya kati katika kupanga, kusimamia utekelezaji, kushirikisha jamii na kuhakikisha chanjo zinapatikana kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa. 


Aidha, ametoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo kutumia maarifa na ujuzi watakaoupata kuimarisha utoaji wa huduma za chanjo katika maeneo yao ya kazi.


Mafunzo hayo ya Wasimamizi wa Ngazi ya Kati (Mid-Level Managers – MLM) yanahusisha Waganga Wakuu wa Mikoa, Waganga Wakuu wa Halmashauri na Makatibu wa Afya kutoka mikoa ya Tabora, Singida, Kagera na Kigoma, na yanatarajiwa kuleta matokeo chanya katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda na ufanisi wa huduma za chanjo nchini.






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com