Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAFANIKIO MAKUBWA HIFADHI YA JAMII: THAMANI YA MIFUKO IMEPAA KUFIKIA SH TRILIONI 24!


Sekta ya Kinga ya Jamii nchini Tanzania imepata mafanikio makubwa ya kihistoria, huku thamani ya mifuko yote ya hifadhi ya jamii ikiongezeka maradufu ndani ya miaka mitano. 

Takwimu mpya zinaonyesha kuwa thamani hiyo imepaa kutoka shilingi trilioni 10.43 mwaka 2020 hadi kufikia shilingi trilioni 24.20 mwezi Desemba 2025.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Clement Sangu, alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Kinga ya Jamii jijini Arusha.

Mbali na mifuko ya hifadhi, Serikali imeimarisha kwa kiasi kikubwa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF). Waziri Sangu ameeleza kuwa katika awamu ya pili ya mpango huo (2020 - 2025), zaidi ya kaya milioni 1.37 zenye watu takribani milioni 5.5 zimenufaika.
Katika kipindi hiki, Serikali imetoa zaidi ya shilingi trilioni 1.55 kama ruzuku kwa kaya walengwa. Aidha, mpango wa ajira za muda umewanufaisha walengwa laki sita (600,000) kwa ujira wa zaidi ya shilingi bilioni 214, hatua iliyoongeza ustahimilivu wa familia hizi dhidi ya majanga ya kiuchumi.

Waziri amebainisha kuwa maboresho ya kisheria yaliyofanyika tangu mwaka 2018 yameleta tija kubwa.

 Idadi ya wanachama katika mifuko ya PSSSF na NSSF imeongezeka kwa asilimia 106 ndani ya miaka mitano tu. Hali kadhalika, uwekezaji wa mifuko hiyo umefikia shilingi trilioni 20.13, ukiwekezwa katika maeneo salama kama hati fungani za Serikali, miliki ardhi, na hisa.
Pia, Waziri aliipongeza mifuko ya WCF na NHIF kwa huduma zao. Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) sasa unahudumia wanachama na wategemezi takribani milioni 6.8, sawa na asilimia 8 ya Watanzania wote, likiwa ni ongezeko muhimu katika kinga ya afya.

Katika mkutano huo uliofanyika ukumbi wa AICC, Waziri Sangu amezindua rasmi Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ya Mwaka 2023 na Hifadhi Skimu. Sera hii mpya inalenga kuleta mwelekeo wa kisasa na kuwajumuisha wananchi ambao kwa muda mrefu walikuwa nje ya mfumo rasmi.

Kupitia NSSF, sasa kundi kubwa la waliojiajiri—ikiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, wachimbaji wadogo, bodaboda na mama lishe—wanaweza kujiunga na "Hifadhi Skimu". Skimu hii imesanifiwa kulingana na mazingira ya vipato vya ambapo wanachama wanaweza kujichangia fedha kidogo kidogo kupitia simu za kiganjani na mawakala wa fedha.

Aidha Mwanachama anaweza kuchangia kwa kurudi nyuma miezi 12 au kulipa mkupuo wa miezi 12 kwenda mbele kulingana na uwezo wake.

Ofisi ya Waziri Mkuu imesisitiza kuwa kinga ya jamii ni silaha muhimu katika kupambana na umaskini unaotokana na uzee, maradhi, na ajali kazini. Kupitia maboresho haya, Serikali inahakikisha kuwa kila Mtanzania, awe amejiriwa au amejiajiri, anapata huduma jumuishi na stahiki za hifadhi ya jamii kuelekea Dira ya 2050.

Kabla ya kufungua mkutano na kuzindua sera na hifadhi, Mhe. Deus Sangu, alitembelea mabanda mbalimbali yaliyopo katika mkutamo huo unmaofanyika AICC.

Akiwa katika banda la Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) alipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, kuhusu Hifadhi ya Jamii kwa Wananchi Waliojiajiri yaani 'Hifadhi Scheme'

Mhe. Sangu alipongeza NSSF kusisitiza kuwa Hifadhi Scheme inaonesha namna ambavyo Serikali inavyowajali wananchi wote hususan waliojiajiri.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com