
Na Bora Mustafa, Arusha .
Jamii ya Ngorongoro kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Ngorongoro jana zilikusanyika katika Kijiji cha Kirtalo, Kata ya Soitsambu, Tarafa ya Loliondo, kwa ajili ya vikao vya maombi maalum, pamoja na mazungumzo ya kijamii yenye lengo la kuliombea eneo hilo amani na kupungua kwa migogoro ya ardhi inayoendelea kujitokeza.
Katika vikao hivyo, wananchi walieleza kuwa migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na msukumo wa kubadilisha matumizi ya ardhi ya jamii, hali ambayo pia imesababisha kuanzishwa kwa matumizi yanayokinzana na shughuli za kijamii na kiuchumi za wakazi wa eneo hilo.
Miongoni mwa matumizi hayo ni pamoja na uanzishwaji wa hifadhi pamoja na shughuli za uwekezaji.
Hata hivyo, washiriki wa vikao vya maombi walisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mazungumzo ya wazi kati ya Serikali, wadau na jamii husika, pamoja na ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi yanayohusu ardhi yao.
Aidha, walieleza kuwa heshima kwa haki za ardhi ya kimila ni nguzo muhimu katika kudumisha amani, mshikamano na ustawi wa jamii.
Kwa upande wake, jamii ilitoa wito kwa Serikali pamoja na wadau wengine kuhakikisha kuwa maamuzi yote yanayohusu matumizi ya ardhi yanazingatia maslahi ya wananchi, ili kulinda maisha, utamaduni na shughuli za uzalishaji za jamii za wafugaji pamoja na wakazi wa Loliondo kwa ujumla.
Jamii hizo pia zimeeleza matumaini kuwa kupitia maombi, mshikamano wa kijamii na majadiliano ya amani, migogoro ya ardhi itaendelea kupungua na maridhiano yataendelea kudumishwa katika Wilaya ya Ngorongoro.


Social Plugin