Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ZAIDI YA WANAFUNZI 500 KUNUFAIKA NA MABWENI MAPYA YA WASICHANA CHUO CHA MAENDELEO YA JAMII MONDULI



Na Jackline Minja MJJWM, Monduli- Arusha

Ujenzi wa mabweni ya wasichana katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Monduli umefikia asilimia 58, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa ya makazi kwa zaidi ya wanafunzi 500 pindi mradi huo utakapokamilika.

Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea mradi huo chuoni hapo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema kukamilika kwa mabweni hayo kutasaidia kulinda usalama wa wanafunzi wa kike na kuwawezesha kusoma katika mazingira salama na tulivu.

“Watoto wakike wako kwenye hatari zaidi wanapolazimika kuishi nje ya maeneo ya Chuo. Kukamilika kwa mabweni haya kutapunguza changamoto za kiusalama na kuwapa wasichana wetu nafasi ya kusoma kwa utulivu na kuzingatia ndoto zao,” amesema Mhe. Mahundi.

Mhe. Mahundi amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya Vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira rafiki ya kujifunzia, hususan kwa masomo ya ufundi na ujuzi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Monduli, Boniface Daniel amesema fedha walizopokea hivi karibuni zitasaidia kuingia awamu ya nne ya ujenzi wa mabweni hayo, hatua itakayoharakisha kukamilika kwa mradi huo.

“Fedha tulizopokea zitatuwezesha kuendelea na awamu ya nne ya ujenzi. Lengo letu ni kuhakikisha mabweni haya yanakamilika kwa wakati ili wanafunzi wengi zaidi wanufaike,” amesema Mkuu wa Chuo Boniface Daniel.

Nao baadhi ya wanafunzi wa Chuo hicho wamepongeza jitihada za Serikali katika ujenzi wa mabweni hayo, wakisema yatasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza morali ya masomo, hasa katika kozi za ufundi.

Katika ziara yake chuoni hapo, Naibu Waziri Mhandisi Maryprisca Mahundi ametembelea madarasa ya ushonaji, eneo la ujenzi wa mabweni hayo pamoja na kufanya mazungumzo na wanafunzi, akiwahimiza kuzingatia nidhamu na kutumia fursa za elimu ya ufundi zinazotolewa na Serikali.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com