Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI WATAKA AMANI KUCHANGAMKIA FURSA NA KULINDA MSHIKAMANO WA KITAIFA

Wakazi na wafanyabiashara wadogo katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani wametoa wito kwa Watanzania wote kudumisha amani na utulivu uliopo nchini, wakibainisha kuwa ndio msingi pekee wa watu kupata riziki na kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi. 

 Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao wamesisitiza kuwa bila amani, shughuli za uzalishaji mali zinakwama, jambo ambalo linaweza kurudisha nyuma ustawi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Kawiya Manyamba, ambaye ni fundi cherehani katika eneo la Maili Moja, amewasihi Watanzania kudumisha amani akitaja kuwa ni tunu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. 

Manyamba ameeleza kuwa uvumilivu na mshikamano ni mambo muhimu yanayowaruhusu wananchi kuendelea na juhudi za kutafuta riziki zao za kila siku, kwani palipo na vurugu, hakuna anayeweza kufanya kazi kwa uhuru. 

 Naye Jabir Makasala, mkazi wa Kibaha Mjini, amewataka Watanzania kuiombea nchi amani akisisitiza kuwa utulivu unamfanya kila mwananchi kuwa huru kufanya shughuli zake za kimaendeleo. 

Amesema kuwa uvunjifu wa amani si jambo la kutamaniwa kwa sababu kila mtu anapenda utulivu uendelee ili kuwe na mshikamano wa dhati katika kuijenga nchi. 

 Kwa upande wake, mjasiriamali Said Ng’ombe amebainisha kuwa amani na mshikamano wa kitaifa ndio kiungo kikuu cha maendeleo ya kiuchumi.

 Ng’ombe amefafanua kuwa bila amani, watu hukosa muda na utulivu wa kufanya shughuli zao za uzalishaji, jambo linalofanya maendeleo kuwa magumu kupatikana, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha kiungo hicho hakivunjiki.

 Wito huu wa wananchi wa Kibaha unakuja wakati ambapo Serikali na wadau mbalimbali nchini wanaendelea kusisitiza umuhimu wa amani kama miundombinu mikuu ya uwekezaji na ukuaji wa uchumi wa viwanda.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com