Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAASISI CCM RUVUMA WATOA WITO WA KUZINGATIA KATIBA NA KUWASIKILIZA WANACHAMA WA NGAZI ZA CHINI

Katibu wa CCM Kata ya Mjini Bi Mikaela Komba akimkabidhi muasisi wa tawi la Mjini Bi Janet Mangula au Mama Mhagama walipomtembelea nyumbani kwake kama ishara ya kuwaenzi waasisi wa chama cha mapinduzi CCM kutambua mchango wao mkubwa katika ujenzi na uhai wa Chama Cha Mapinduzi
Bi Marry Nyanjako muasisi wa CCM kutoka Tawi la Mashujaa kata ya mjini akiwa amekaa nyumbani kwake baada ya kutembelewa na viongozi wa kata ya mjini ukiongozwa na Diwani wa Kata hiyo Mathew Ngalimanayo pichani hayupo

Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma

Waasisi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma wamewataka wanachama na viongozi wa chama hicho kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni za CCM ili kukiendeleza na kukilinda chama, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea maadhimisho ya miaka 49 tangu kuanzishwa rasmi kwa CCM tarehe 5 Februari 1977.

Wito huo umetolewa wakati wa ziara za kuwatembelea waasisi wa chama katika matawi yao mbalimbali ndani ya Manispaa ya Songea, hususan Kata ya Mjini.

Muasisi wa CCM Bi. Marry Nyanjako amesema chama hakina tatizo bali changamoto zinatokana na wanachama na viongozi kushindwa kuzingatia misingi ya Katiba, Sheria na Kanuni za chama.

Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi kubwa anazozifanya kukiongoza chama na taifa, huku akisisitiza umuhimu wa viongozi kushuka chini kuwasikiliza wanachama na kutatua kero zao.

Bi. Marry amekumbusha desturi za zamani enzi za Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo maadhimisho ya CCM yalihusisha kusikiliza wananchi moja kwa moja, akisisitiza kuwa chama huanzia ngazi za chini na ndipo hupatikana suluhisho la changamoto zake.

Kwa upande wake, Mzee Ndauka, muasisi wa CCM kutoka Tawi la Mahenge C, amesema kuwa chimbuko la CCM na maendeleo ya taifa lipo chini, hivyo mabalozi wa mashina na viongozi wa msingi wana wajibu mkubwa wa kulinda amani na mshikamano wa nchi.

Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anajitahidi kwa kiwango kikubwa, lakini mafanikio ya juhudi hizo yanategemea ushirikiano wa viongozi wa ngazi za chini kwa kutekeleza Ilani ya CCM, kufanya vikao vya mara kwa mara na kufuatilia wageni wanaoingia na kutoka katika maeneo yao.

Katika kuonesha mshikamano na kuthamini mchango wa waasisi, uongozi wa CCM Kata ya Mjini ukiongozwa na Katibu wa Kata hiyo Mikaela Komba pamoja na Diwani wa Kata ya Mjini, Mathew Ngalimanayo, uliwakabidhi zawadi waasisi wa chama kama ishara ya upendo, heshima na kutambua mchango wao mkubwa katika ujenzi na uhai wa Chama Cha Mapinduzi.Katibu wa kata ya mjini Bi Mikaela Komba Akizungumza baada ya kumkabidhi muasisi wa chama cha mapinduzi CCM tawi la Mpambalioto iliyopo katika Kata ya Mjini

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com