Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIJANA 70 MASASI WANUFAIKA NA MRADI WA BRIDGE TANZANIA CHINI YA UNESCO NA JAMHURI YA KOREA

Na mwandishi wetu Malunde 1-Blog-Masasi 

Vijana 70 kutoka Wilaya ya Masasi wameanza kunufaika na mradi wa Bridge Tanzania unaotekelezwa chini ya UNESCO kwa ufadhili wa Jamhuri ya Korea, kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. 

Mafunzo hayo yatadumu kwa kipindi cha miezi mitatu na yatafanyika katika vituo viwili vya Chiungutwa na Lupaso. 

Mgeni rasmi katika uzinduzi wa mafunzo hayo ni  ndugu James Chitumbi, mkuu wa divisheni ya kilimo, mifugo na uvuvi Masasi, aliyemwakilisha Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, ndugu Alphaxard Etanga, ambapo amesisitiza kuwa vijana hao hawataachwa bali watapewa tafsiri pana ya mradi mama ili wanufaike kikamilifu.

Akizungumza katika hafla hiyo, mkurugenzi wa idara ya elimu mbadala na watu wazima Zanzibar, Bi. Mashavu Ahmad Fakihi, amesema mradi wa Bridge ni “daraja” linalokwenda kuwavusha vijana kutoka giza kwenda mwanga kwa kuwawezesha kuona na kutumia fursa mbalimbali zilizopo nchini. 

Ameipongeza UNESCO na Jamhuri ya Korea kwa kuja na mradi huo muhimu, akibainisha kuwa ni sehemu ya ukombozi mkubwa wa vijana na suluhisho la changamoto ya ajira.

 Amewahimiza wanufaika kutumia fursa hiyo adimu kwa bidii na kujifunza kwa dhati ili kujijengea mustakabali bora.

Bi. Fakihi ameeleza kuwa mradi umezingatia mazingira ya eneo husika kwa kutoa mafunzo ya stadi kama ubanguaji wa korosho, ufugaji na kisomo, akisisitiza kuwa kusoma, kuandika na kuhesabu ni msingi wa taaluma yoyote. 

Ametaja pia ufundi wa bodaboda kama fursa ya kiuchumi kwa vijana, na kuongeza kuwa mradi unaendana na sera na mipango ya serikali pamoja na ilani ya chama tawala inayowapa vijana kipaumbele. 

Amebainisha kuwa mradi huo unatekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo Zanzibar wana vituo viwili Kaskazini kutokana na changamoto ya awali ya watu wasiojua kusoma, licha ya sasa kufikia kiwango cha asilimia 90.6 cha watu wanaojua kusoma.

Kwa upande wa wakufunzi, Bi. Neema Lookmai na Mwalimu Salumu Njalau, ambao ni miongoni mwa waanzilishi wa mradi wa Bridge Tanzania chini ya UNESCO, wamesema wako tayari kufundisha kwa moyo wote ili kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa. 

Wamesema wana imani kubwa kuwa vijana watatumia ujuzi na maarifa watakayoyapata kuanzisha vikundi vya wajasiriamali, vikoba na shughuli za kujitegemea kiuchumi, hivyo kuchangia maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com