Tume ya taarifa ya ulinzi wa Taarifa binafsi Tanzania PDPC imetangaza kuanza mara moja kwa ukaguzi wa uzingatiaji wa sheria kwa Taasisi za umma na za binafsi, zinazokusanya na kuchakata taarifa binafsi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Januari 22, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo Dkt. Emmanuel Mkilia amesema zoezi hilo linafanyika mara baada ya muda wa hiari kuisha kulingana na tangazo la Tume hiyo lililoweka ukomo wa Aprili 8, 2026 kwa Taasisi husika kukamilisha usajili wao.
"Ukaguzi huu utahusisha kubaini Taasisi za umma na za binafsi zinazokusanya, kuhifadhi kuchakata na kusafirisha taarifa binafsi nje ya nchi bila kuzingatia matakwa ya sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi sura ya 44 na kanuni zake na PDPC tutachukua hatua kali za kisheria dhidi ya yeyote, taasisi ama kampuni itakayokiuka sheria hii ikiwa ni pamoja na faini, kifungo, fidia kwa waathirika ama vyote kwa pamoja." Amesema Dkt. Mkilia.
Aidha PDPC imesema mtu ama Taasisi itakayobainika kutumia taarifa ya mtu binafsi bila ridhaa yake au kinyume na taratibu zilizowekwa kisheria, Taasisi hiyo itawajibishwa Ipasavyo bila ya kujali hadhi ama ukubwa wa Taasisi itakayokiuka misingi ya sheria katika ulinzi wa taarifa binafsi.
Pamoja na mafanikio yanayotokana na ukuaji wa TEHAMA duniani, kumekuwepo na changamoto mbalimbali ikiwemo ulinzi wa taarifa binafsi ambazo zimekuwa zikikusanywa, zikichakatwa na wakati mwingine kusafirishwa kutoka nchi moja kwenda nyingine bila kuzingatia utaratibu na misingi ya ulinzi wa taarifa binafsi iliyokubalika kisheria.



Social Plugin