Uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuunda Tume ya Maridhiano ya Kitaifa, kama alivyotangaza katika hotuba yake ya kuukaribisha mwaka 2026, ni hatua ya kimkakati inayolenga kuiponya nchi kutokana na majeraha ya kisiasa na kijamii.
Katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaelekea katika mzunguko mwingine wa kisiasa, maridhiano si chaguo bali ni hitaji la lazima ili kuhakikisha taifa linabaki kuwa kitu kimoja. Maana ya hatua hii kwa mwaka 2026 ni kuweka msingi wa kuaminiana kati ya serikali, vyama vya siasa, na wananchi, ili tofauti za kiitikadi zisiwe chanzo cha mpasuko bali ziwe chachu ya ujenzi wa demokrasia iliyokomaa.
Pamoja na kauli hiyo ya upole bado kuna baadhi ya watu katika mitandao waliendelea kutoa maoni ya dhihaka, matusi ya nguoni, na lugha za kashfa ikiwa ni kielelezo cha mmomonyoko wa maadili na ukosefu wa staha ambao unahatarisha jitihada hizi za kuwa na taifa lenye utulivu na amani.
Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa badala ya kujadili muundo na majukumu ya tume hiyo kwa hoja, baadhi ya watu wanatumia uhuru wa maoni kupandikiza mbegu za chuki na utengano. Hali hii inathibitisha kuwa ukombozi wa fikra unahitajika kwa haraka ili jamii itambue kuwa matusi si suluhu ya changamoto za kisiasa.
Kwa upande mwingine, sauti za busara zinazowahimiza vijana kulinda amani na kutumia mazungumzo badala ya vurugu ndizo zinazopaswa kupewa kipaumbele.
Tukio la tarehe 29 Oktoba linapaswa kubaki kama funzo la kudumu kuwa amani ikishapotea, gharama ya kuirejesha ni kubwa mno. Maridhiano ya kweli hayawezi kufikiwa ikiwa upande mmoja unatoa mkono wa heri huku upande mwingine ukiwa umejaza matusi na kashfa viganjani. Ni lazima vijana watambue kuwa wao ndio walinzi wa urithi wa Tanzania, na kutumiwa kama vyombo vya kuchochea taharuki ni kujihujumu wenyewe na vizazi vijavyo.
Jukumu la viongozi wa dini na taasisi za kijamii katika kipindi hiki ni kuwa daraja la kweli la upatanisho. Tunahitaji sauti zinazounganisha raia na viongozi wao, si kuta zinazowatenganisha.
Mwaka 2026 unapaswa kuwa mwaka wa ukomavu, ambapo maridhiano yanatazamwa kama fursa ya kurekebisha makosa ya nyuma na kuimarisha mshikamano.
Tanzania ni nyumba yetu sote, na ujenzi wa nyumba hii unategemea utulivu, heshima kwa mamlaka, na uwezo wetu wa kukaa meza moja na kukubaliana kutokubaliana bila kutukanana. Huu ndio wakati wa kuweka nchi kwanza na kuacha siasa za chuki ambazo hazina tija kwa maendeleo ya taifa letu.
Social Plugin