Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Tanzania na Marekani zimeonyesha dhamira ya kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu katika sekta ya teknolojia na madini, hasa katika utafiti wa Madini ya Kinywe, hatua inayolenga kuongeza tija, kufungua fursa za ajira na kuimarisha maendeleo ya kiteknolojia kwa pande zote mbili.
Akizungumza jijini Dodoma Januari 21, 2026, Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde, amesema ushirikiano huo unalenga kutumia teknolojia ya kisasa katika utafiti wa madini, kubaini rasilimali zilizopo, na kufanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa madini yenye mahitaji makubwa duniani.
“Tuko hapa kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani katika teknolojia na sekta ya madini. Tunaamini kupitia mpango huu, pande zote zitanufaika, hasa ikizingatiwa Tanzania ina fursa kubwa katika teknolojia na nishati,” amesema Mavunde.
Ameeleza kuwa Serikali ya Marekani imeonyesha utayari wa kupanua wigo wa ushirikiano katika sekta ya madini, hususan katika utafiti wa kina, ili kubaini rasilimali zilizopo na fursa za uwekezaji zinazoweza kuendeleza uchumi wa ndani.
Mavunde amesisitiza kuwa Tanzania na Marekani zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu katika nyanja za maendeleo na usalama, huku Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zilizonufaika na misaada ya Marekani katika sekta za afya, elimu, kilimo na usalama wa chakula.
“Tunaishukuru Marekani kwa kuendelea kushirikiana nasi katika kukuza uchumi na ustawi wa wananchi, ikiwemo kupitia rasilimali na sekta muhimu za uzalishaji,” amesema Waziri Mavunde.
Ameongeza kuwa kupitia Wizara ya Madini na Wizara ya Nishati ya Marekani, zimeandaliwa programu maalum zitakazosaidia utekelezaji wa ajenda za maendeleo, hususan katika kuendeleza sekta ya madini na ujenzi wa uwezo wa wataalamu wa ndani.
“Tanzania inafahamika kimataifa kwa kuwa na madini yenye mahitaji makubwa, hali inayofanya ushirikiano huu kuwa fursa muhimu ya kujenga uwezo wa Watanzania, hususan katika utafiti wa kisasa wa kijiolojia,” ameongeza.
Waziri Mavunde pia amebainisha kuwa zipo leseni za uchimbaji zinazomilikiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), ambapo kupitia ushirikiano huu, kutafanyika utafiti wa pamoja kubaini maeneo yenye uwekezaji mkubwa na rasilimali zenye tija zaidi.
Utafiti huo unatarajiwa kusaidia Serikali kupata takwimu sahihi za rasilimali zilizopo, hususan katika mikoa ya Lindi na Mtwara, ambako dalili za uwepo wa Madini ya Kinywe tayari zimeshapatikana, huku mipango ikiwa ni kupanua zaidi eneo la utafiti.
Serikali ya Marekani imeeleza utayari wake wa kuongeza eneo la utafiti, hasa katika utafiti wa kina wa Madini ya Kinywe, ili kuhakikisha Tanzania inanufaika ipasavyo na rasilimali hizo.
“Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Marekani katika sekta ya madini na maeneo mengine ya kimkakati kwa lengo la kuimarisha uchumi wa Taifa na kuongeza manufaa kwa wananchi,” amesema Mavunde.
Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andy Lentz, amesema ushirikiano huu ni kielelezo cha uhusiano thabiti kati ya pande zote mbili katika kukuza maendeleo ya kiuchumi na kiteknolojia.
Amesema mpango wa utafiti wa Madini ya Kinywe utawezesha kubaini rasilimali kwa usahihi, kuongeza uwekezaji na kuunda fursa mpya za ajira kwa wananchi wa Tanzania.
Balozi Lentz ameongeza kuwa Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi ya maendeleo, ikiwemo kutoa mafunzo ya kitaalamu na kubadilishana uzoefu katika teknolojia ya madini, hatua itakayoongeza uwezo wa wataalamu wa ndani na kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.





Social Plugin