Na Regina Ndumbaro Tunduru -Ruvuma
Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru (TAMCU LIMITED) kimehitimisha rasmi mnada wa korosho wa msimu huu leo tarehe 2 Januari 2026, katika ukumbi wa Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma.
Mnada huo ulikuwa ni wa nane na wa mwisho tangu kuanza kwa minada ya korosho msimu huu, huku ukihusisha wanunuzi na wadau mbalimbali wa zao hilo muhimu la biashara.
Akizungumza katika mnada huo, Mwenyekiti wa TAMCU Limited, Bwana Mussa Manjaule, amesema kuwa kwa daraja la juu (standard grade), bei ya juu ya korosho imefikia shilingi 2,560 kwa kilo, huku bei ya chini ikiwa shilingi 2,310.
Hali hiyo imefanya bei ya wastani kwa daraja hilo kufikia shilingi 2,480, jambo linaloonyesha mwenendo mzuri wa soko la korosho msimu huu.
Kwa upande wa daraja la chini, Manjaule ameeleza kuwa korosho zimeuzwa kwa bei ya juu ya shilingi 1,790 na bei ya chini ya shilingi 1,710 kwa kilo, na hivyo kufanya bei ya wastani kuwa shilingi 1,761.
Amebainisha kuwa licha ya tofauti za madaraja, wakulima wameendelea kunufaika na minada hiyo kupitia bei shindani.
Aidha, Mwenyekiti huyo amewataka wakulima wa korosho wilayani Tunduru na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla kuanza maandalizi mapema kwa msimu ujao kwa kusafisha mashamba na kuyaweka katika hali ya utayari.
Amesisitiza kuwa maandalizi hayo yatasaidia korosho kuzaliana kwa wingi na kuongeza tija na kipato cha wakulima katika msimu ujao wa uzalishaji.




Social Plugin