Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

POLISI NJOMBE WAKANUSHA TAARIFA ZA ASKARI KUCHOMWA MOTO NA KUPORWA SILAHA



Na mwandishi wetu,Njombe

Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe katika taarifa yake kwa Vyombo vya habari limekanusha taarifa zilizokuwa zimesambazwa katika Mitandao ya Kijamii nchini zikiambatana na picha mjongeo (Video), zikieleza uwepo wa Askari Polisi wa Mkoa huo aliyechomwa moto na kisha kuporwa silaha Mkoani humo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Mahamoud Banga, Januari 28, 2026 amesema kuwa katika Mkoa wa Njombe hakuna tukio kama hilo, akionya dhidi ya wanaoandaa na kusambaza taarifa za uongo na upotoshaji.

"Jeshi la Polisi linatoa wito kwa baadhi ya wananchi wenye tabia za kuandaa na kusambaza taarifa za uongo na upotoshaji kwa njia mbalimbali kuacha kwani ni kinyume cha sheria za nchi na maadili ya Mtanzania na hakuna faida yoyote kwa wanaofanya hivyo pamoja na familia zao na kwa jamii kwa ujumla." Amesema Kamanda Banga.

Polisi pia imesema inaendelea kumfuatilia mtu ama watu waliochukua na kutumia picha mjongeo ya tukio la zamani ambalo askari walikwenda kutoa msaada kwa wananchi na kutengenezea taarifa hiyo ya uongo na kisha kuisambaza katika mitandao ya kijami

Aidha Kamanda Banga amesema Polisi wanaendelea kutekeleza majukumu yao kwa kushirikiana na wananchi kupitia programu za Polisi Jamii ili kubaini na kuzuia uhalifu sambamba na kufanya doria, misako na operesheni katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha maisha na mali za wananchi zinakuwa salama wakati wote.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com