Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MAKONDA AAHIDI BILIONI MOJA KWA WAANDISHI WA MITANDAONI


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, ameahidi kuomba Serikali kutenga kiasi cha shilingi bilioni moja hadi bilioni mbili kwa ajili ya kuwawezesha waandishi wa habari za mitandaoni nchini kukopeshwa fedha zitakazowawezesha kununua vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi, kwa lengo la kuboresha ubora wa maudhui na kuitangaza Tanzania kimataifa.

Waziri Makonda ametoa ahadi hiyo Januari 13, 2026, wakati akizungumza na watumishi wa Wizara hiyo katika Ofisi za Wizara zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, sambamba na hafla ya makabidhiano ya Ofisi kati yake na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, Mheshimiwa Profesa Palamagamba Kabudi.

Amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa vijana waliojiajiri kupitia vyombo vya habari vya mtandaoni, hususan televisheni za mtandaoni (Online TV) na mitandao ya kijamii, hivyo kuna haja ya kuwawezesha ili wafanye kazi zao kwa viwango vinavyokubalika kimataifa.

“Mungu akituwezesha, vijana wengi wamejiajiri kwenye habari, hasa kupitia televisheni za mtandaoni na mitandao ya kijamii. Tutaomba mamlaka husika, na mtakumbuka Mheshimiwa Rais anapenda sana mitandao ya kijamii, hata alipoingia madarakani alihakikisha vijana wanapata ajira,” amesema Mhe. Makonda.

Ameongeza kuwa atamwomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutenga fedha hizo ili ziwe mikopo kwa waandishi wa mitandaoni, akisisitiza kuwa lengo ni kuboresha ubora wa kazi zao.

“Nitaenda kumlilia Dkt. Samia ili atupatie fedha kiasi cha shilingi bilioni moja hadi bilioni mbili ili tuwakopeshe vijana wa mitandaoni wawe na vifaa vyao wenyewe. Lengo ni kuhakikisha hawarekodi kwa simu pekee, bali wanatumia kamera za kisasa, wanakuwa na kompyuta bora na kutengeneza maudhui ambayo dunia itayaona na kuiona Tanzania katika uzuri wake,” ameeleza.

Katika hatua nyingine, Waziri Makonda amesema Wizara hiyo ina mpango wa kuanzisha Kitengo maalum cha Mawasiliano ya Lugha za Kimataifa kitakachohusika na kuandaa na kusambaza habari za matukio muhimu ya kitaifa kwa vyombo vya habari vya kimataifa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com