Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeendelea kutoa elimu ya hifadhi ya jamii na kuandikisha wanachama wapya kupitia kampeni ya NSSF Staa wa Mchezo Paka Rangi, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, ameongoza zoezi hilo katika Soko la Mabibo, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na wananchi na wafanyabiashara wa soko hilo pamoja na wakazi wa maeneo ya jirani, Bw. Mshomba alisema lengo la kampeni hiyo ni kuhamasisha wananchi, hususan waliojiajiri, kujiunga na kuchangia NSSF ili kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa na Mfuko, yakiwemo pensheni ya uzeeni, urithi, ulemavu, uzazi na matibabu.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita imetoa fursa kwa kila Mtanzania aliyejiajiri kujiunga na kuchangia NSSF kwa hiari, jambo ambalo halikuwepo hapo awali, hivyo kuwataka wananchi kutumia fursa hiyo muhimu ya kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha yao ya sasa na ya baadaye.
Bw. Mshomba alibainisha kuwa mwanachama atakayejiunga na kuchangia kwa kipindi cha miezi mitatu mfululizo, ataanza kunufaika na mafao ya muda mfupi, yakiwemo ya matibabu na uzazi.
Aidha, alisema Mfuko umeweka utaratibu rafiki wa uchangiaji unaomuwezesha kila mwananchi kuchangia kulingana na uwezo wake, ambapo anayechangia shilingi 30,000 kwa mwezi atanufaika na mafao yote, na anayechangia shilingi 52,200 kwa mwezi atanufaika yeye pamoja na mwenza wake na wategemezi wasiopungua wanne.
Aliongeza kuwa michango inaweza kutolewa kwa utaratibu wa kila siku, kila wiki, kila mwezi au kwa msimu, na kwamba mwanachama anaweza kujichangia popote alipo kwa kutumia simu ya mkononi, huku wategemezi wake wakiendelea kunufaika na mafao ya mirathi endapo atafariki dunia.
Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wa Mfuko, Kaloli Godfrey alisema walijiunga kama kikundi cha watu 48 na wamekuwa wakinufaika na mafao mbalimbali, yakiwemo ya matibabu, jambo lililowahamasisha kuendelea kuchangia.
Kwa upande wake, Ali Hassan, Kaimu Meneja wa Soko la Mabibo, pamoja na mfanyabiashara wa nyanya Alex Emanuel, waliishukuru NSSF kwa kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii sokoni hapo, wakisema kuwa mwamko wa wananchi kujiunga na kuchangia umeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Kwa nyakati tofauti, Mameneja wa NSSF wa Mkoa wa Kinondoni, Temeke, Ilala na Ubungo waliwahamasisha wananchi na wafanyabiashara wa Soko la Mabibo kutumia fursa zilizopo kujiunga na kuchangia katika Mfuko huo.





















Social Plugin