Na Sumai Salum – Kishapu
Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imepanda jumla ya miti 1,500 katika Shule ya Msingi Isoso, Kata ya Kishapu, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, yenye kauli mbiu isemayo "Uzalendo ni kutunza mazingira, shiriki kupanda miti".
Akizungumza kwa niaba ya Mgeni Rasmi Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Bi. Fatma H. Mohamed, amesema upandaji wa miti ni suala la msingi katika kulinda mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuhakikisha kizazi cha sasa na kijacho kinaishi katika mazingira salama na endelevu.
Fatma amebainisha kuwa maadhimisho hayo yamebeba ujumbe mahsusi wa kuenzi maono ya Rais Samia ya kulinda mazingira na kuhimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika upandaji na utunzaji wa miti, akisisitiza kuwa kupanda mti mmoja ni kuwekeza maisha ya baadaye.
Kwa upande wake Mhifadhi Misitu wilayani humo, Tumaini Masatu amesema wakala huo umeendelea kuwa mstari wa mbele katika kampeni za uhifadhi wa misitu na utoaji wa elimu ya mazingira, hususa kwa wanafunzi ili kujenga kizazi chenye uelewa na uwajibikaji wa mazingira.
Masatu amefafanua kuwa miti iliyopandwa itasaidia kuboresha mazingira ya shule, kutoa kivuli, kupata matunda, kupunguza athari za ukame pamoja na kuongeza uelewa wa wanafunzi juu ya umuhimu wa rasilimali za misitu.
Naye Mkuu wa Shule ya Msingi Isoso Gilbert Mtunguja ameushukuru uongozi wa Wilaya na TFS kwa kuchagua shule hiyo kuwa sehemu ya maadhimisho, akiahidi kuwa shule itahakikisha miti yote iliyopandwa inatunzwa ipasavyo.
Maadhimisho hayo yamehitimishwa kwa zoezi la pamoja la upandaji miti likiwahusisha viongozi,wakuu wa Taasisi, watumishi wa Halmashauri, TFS, walimu, wanafunzi na wananchi, ikiwa ni ishara ya mshikamano na dhamira ya dhati ya kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kulinda na kuhifadhi mazingira nchini yakiambatana na kauli mbiu isemayo "Uzalendo ni kulinda mazingira, shiriki kupanda miti".
Social Plugin