Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MFUMO WA BWANA NA BIBI BOOM KUPUNGUZA GHARAMA ZA MIKOPO KWA ASILIMIA 60



Na Josephine Manase, Dodoma

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imezindua mfumo wa kidijitali wa huduma kwa wateja uitwao Bwanaboom na Bibiboom, unaotumia akili mnemba (AI) kutoa majibu ya papo kwa papo kwa wanafunzi na wazazi, hatua inayotarajiwa kupunguza gharama za huduma za mikopo kwa takribani asilimia 60.

Mfumo huo umeunganishwa moja kwa moja na mifumo ya mikopo ya HESLB, hivyo kupunguza safari zisizo za lazima, foleni ndefu na malalamiko ya wanafunzi.

 Akizungumza Januari 28, 2026, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) wa HESLB, Bahati Singa, amesema awali bodi iliweza kuwahudumia walengwa 5,000 hadi 6,000 kwa wakati mmoja, lakini sasa mfumo una uwezo wa kuhudumia zaidi ya walengwa 10,000, kwa lengo la kufikia hadi 200,000 kadri matumizi yanavyoongezeka.

“Mteja anauliza swali na anapata jibu papo hapo bila kusubiri siku au kufika ofisini,” amesema Singa, akiongeza kuwa mfumo huo utaongeza ufanisi na kupunguza mzigo wa huduma kwa wateja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Bill Kiwia, amesema hatua hiyo itasaidia kuondoa changamoto ya wingi wa maswali na maombi yaliyokuwa yakikabili bodi. “Mfumo huu utaondoa malalamiko mengi na kuharakisha huduma kwa wateja wetu,” amesema.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, amesema mfumo huo utaimarisha uwazi na uwajibikaji, akiwahimiza Watanzania kuutumia. 

“Ni hatua ya kujivunia kuona HESLB ikianzisha mfumo wake wa kidijitali,” amesema.

Wanafunzi na wazazi wamepokea hatua hiyo kwa matumaini, wakisisitiza umuhimu wa ulinzi wa taarifa binafsi na ushirikishwaji wa watu wenye mahitaji maalum. Backline Humbaro, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), amesema mfumo huo utapunguza gharama, muda na msongo wa mawazo kwa wanafunzi walioko mbali na ofisi za bodi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com