
Utoaji wa mikopo ya shilingi bilioni moja isiyo na riba katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui mkoani Tabora kwa ajili ya vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu ni kielelezo tosha cha namna Serikali ya Awamu ya Sita ilivyodhamiria kuwakwamua wananchi wake kutoka kwenye lindi la umaskini.
Hatua hii iliyofikiwa na Halmashauri ya Uyui kwa kuwafikia wanufaika zaidi ya elfu moja kupitia vikundi mbalimbali, inatoa picha pana ya nini kitatokea nchini ikiwa halmashauri zote 184 nchini Tanzania zitatekeleza sheria hii ya asilimia kumi kwa uadilifu na kasi ileile.
Ikiwa mfumo huu utakuwa ni utamaduni wa kila halmashauri, maana yake ni kwamba mabilioni ya shilingi yatasambazwa kila mwaka moja kwa moja mikononi mwa vijana wabunifu, litabadilisha taswira ya mitaa yetu kutoka maeneo ya kulalamika ukosefu wa ajira na kuwa vitovu vya uzalishaji na biashara ndogondogo.
Utekelezaji wa sheria hii nchi nzima una maana kubwa kwa ukuaji wa pato la taifa kwani unabadilisha kundi kubwa la vijana kutoka kuwa wategemezi na kuwa walipakodi na wazalishaji mali.
Vijana wanapopata mitaji isiyo na riba, wanapata uwezo wa kuanzisha miradi ya ufugaji, kilimo cha kisasa, na viwanda vidogo ambavyo vinazalisha bidhaa zinazohitajika sokoni. Hali hii inatengeneza mnyororo wa thamani ambapo fedha za ndani ya halmashauri zinazunguka ndani ya jamii ileile na kurudi kama marejesho ili kusaidia wengine, jambo linalofanya uchumi wa vijana kuwa endelevu.
Kwa msingi huo, juhudi za viongozi wa Uyui kama Afisa Maendeleo ya Jamii Amoniche Mtweve na Mwenyekiti wa Halmashauri Shabani Katalambula, zinapaswa kuwa somo kwa maeneo mengine kuwa mikopo hii si ruzuku ya bure bali ni mbegu ya kiuchumi inayopaswa kulelewa ili kuzaa matunda ya maendeleo kwa taifa zima.
Athari za kijamii na kiuchumi za sera hizi ni kubwa kwani zinasaidia kupunguza matumizi ya nguvu kazi ya taifa katika mambo yasiyo na tija na badala yake kuelekeza nguvu hiyo kwenye uzalishaji mali.
Vijana wanapokuwa na shughuli rasmi za kiuchumi, amani ya nchi inaimarika na kiwango cha uhalifu kinashuka kwa kiasi kikubwa. Maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifanya kila halmashauri kuwa kitovu cha maendeleo yanatimia pale tunapoona akina Masanja Mrisho na Sada Katamata wakishuhudia namna mikopo hiyo ilivyokuwa nguzo ya biashara zao. Hii ndiyo Tanzania tunayoitaka, ambapo serikali inatoa fedha na wakati huo huo inatengeneza mfumo wa kikodi unaomlinda mzalishaji ili aweze kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi.
Ukuaji wa uchumi wa vijana nchini unategemea sana uthubutu wa viongozi wa ngazi za chini kusimamia fedha za umma na kuzielekeza kwenye miradi yenye tija kama inavyofanyika Uyui. Ikiwa kila mkurugenzi wa halmashauri na kila afisa maendeleo atahakikisha asilimia kumi inawafikia walengwa kwa wakati, umaskini utabaki kuwa historia nchini Tanzania. Uhusiano wa karibu kati ya uwekezaji wa viwanda na mikopo ya vikundi ndio utakaolifikisha taifa kwenye uchumi wa kati wa juu uliokusudiwa.
Social Plugin