Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAMILIKI WA BOTI KUTOKA MKOANI KAGERA NA GEITA WAMEKUTANA WILAYANI MULEBA KUJADILI CHANGAMOTO ZAO




Katibu wa wamiliki wa both za abiria kwa baadhi ya visiwa vya Kagera na Geita, Masudi Ibrahim Masudi akizungumza

Afisa Mfawidhi wa TASAC Mkoa wa Geita akizungumza na wamiliki wa vyombo vya majini Boti kutoka Mkoa wa Kagera na Geita

Mwenyekiti wa kikundi cha usafirishaji wa Boti na mizigo ya abiria Magarini, Chaina Bernado Katainawabo akizungumza

*****

Na Mbuke Shilagi Kagera

Wamiliki wa vyombo vya majini kutoka Muleba Mkoani Kagera na Chato Mkoani Geita wamekutana na wadau Wilayani Muleba kujadili changamoto wanazokumbana nazo majini wanapokuwa katika shughuli zao.

Wakizungumza katika Mkutano uliofanyika katika Kitongoji cha Magarini Kata ya Nyakabango Wilayani Muleba  Katibu wa wamiliki boti za abiria kwa baadhi ya visiwa vya Kagera na Geita, Masudi Ibrahimu Masudi na Mwenyekiti wa kikundi cha usafirishaji wa boti na mizigo ya  abiria Magarini Bw. Chaina Bernado Katainawabo wamesema kuwa kumekuwepo changamoto ya kukamatwa kwa baadhi ya Boti ndani ya maji jambo ambalo limeweza kupelekea usalama kuwa mdogo kwa abiria na mizigo kutokana na taharuki.

Wameeleza kuwa wamekuwa wakipokea malalamiko kwa wanakikundi wao kwa kukamatwa kwa Boti zao ndani ya maji ili kukaguliwa endapo wamebeba samaki wachanga jambo ambalo wao wamependekeza kukaguliwa wakati wakiwa nchi kavu au wakati wakiwa wanashusha abiria na mizigo kuliko majini ambako usalama unakuwa ni mdogo.

Kwa upande wake mmiliki wa boti ya Mv. Tawakali  Bw. Idd Deogratius ameeleza kuwa tozo za Bandari zimekuwa juu kutoka 7,500 kwa mwaka 2023 mpaka 30,000 kwa mwezi wa 12,2025 kwa kenta moja ya mabanzi 170-180 huku akiomba kupunguzwa kwa tozo hizo ili kuzimudu.

Aidha changamoto nyingine waliobainisha ni kutokuwa na taa katika gati wanazotumia nyakati za usiku jambo linalopelekea kusumbuka usiku na wakati mwingine kupoteza simu zao majini na abiria kuanguka majini wanaposhuka huku wakiomba serikali kuweka miundombinu rafiki kwa nyakati zote.

Naye Afisa Mfawithi wa Tasac Mkoa wa Geita Bw. Godfrey Chegele ameeleza kuwa kikao hicho ni cha kuelezana na kutatua changamoto baina yao kwa kuangalia usalama kwa pande zote kwa mujibu wa sheria na taratibu pamoja na busara pale ambapo chombo kipo ndani ya maji kitakuwa katika mazingira ambayo sio salama.

Amebainisha kuwa katika jitihada za kupunguza au kumaliza kabisa vifo ndani ya maji Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan imehakikisha usalama ndani ya maji unaimarika kwa kutoa Boti kwa utafutaji na uokozi na kwamba kila anayefanya kazi ndani ya maji anakuwa salama.









Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com