
Kiwanda cha kuzalisha mchele kilichopo Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga, kinachomilikiwa na mwekezaji Mtanzania aliyewekeza zaidi ya shilingi bilioni 100, ni miongoni mwa miradi mikubwa ya uwekezaji wa ndani hapa nchini.
Mradi huu ulisajiliwa na Mamalaka ya Uwekezaji na umefanikiwa kupata vivutio mbalimbali vya kikodi, ikiwemo msamaha wa ushuru wa forodha kwa rasilimali za mtaji kama vile mitambo, mashine, vichwa vya malori pamoja na nondo (iron steel) zilizotumika katika ujenzi wa kiwanda.Mradi huu unatekelezwa katika eneo lenye ukubwa wa jumla ya hekari 54.
Mapema leo, mwekezaji ametembelewa na timu kutoka Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania kwa lengo la kujionea maendeleo ya mradi huo. Ziara hiyo ni sehemu ya ushuhuda unaotolewa wakati wa utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani inayoendelea nchini.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa mradi huo, Dkt. Jesca Kabelwa, amesema kuwa hadi sasa mradi umeajiri wafanyakazi 55, ambao wengi wao ni Watanzania. Ameeleza kuwa mradi ulisajiliwa rasmi mwaka 2024 na ulianza uzalishaji mwezi Januari 2026.
Dkt. Jesca Kabalwa ameongeza kuwa ushirikiano na Mamlaka ya Uwekezaji umewezesha kutekeleza mradi kwa urahisi zaidi, hususan kupitia kupata unafuu wa mtaji kwa kutumia vivutio vya uwekezaji vilivyotolewa na Serikali.
Aidha, amesema kuwa wakulima wadogo wa Mkoa wa Shinyanga wananufaika moja kwa moja na mradi huo, kwani kiwanda kimekuwa kinanunua zao la mpunga kutoka kwao, hatua inayochangia kuongeza kipato cha wakulima na kuleta maendeleo endelevu katika sekta ya kilimo mkoani humo.








Social Plugin