Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ILALA TUNAJIVUNIA RAIS SAMIA, AMETULETEA MAENDELEO- MAMBO


Na Jonas Jovin, Dar

Wananchi wa Wilaya ya Ilala Jijini Dar Es Salaam wameeleza kufurahishwa na kazi kubwa inayotekelezwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hasa katika Ujenzi wa mundombinu ya barabara za ndani, Vyumba vya madarasa katika shule za msingi na Sekondari pamoja na ujenzi wa miundombinu katika sekta ya afya na maji Wilayani humo.

Kwa kuitaja, wananchi hao wameeleza kuhusu ujenzi wa barabara za ndani kupitia miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mradi wa DMDP, ikiwemo barabara ya Nyeburu- Miti mirefu pamoja na barabara ya Kigezi- Njianne kuelekea Majohe, wakisema awali ilikuwa ni ngumu kuona barabara za ndani zikijengwa kwa kiwango cha lami nchini.

Bw. Othman Hassan Mambo, Mkazi wa Nyeburu, ameitaja miradi ya ujenzi wa madarasa katika shule za msingi na sekondari ikiwemo katika shule za Msingi Nyeburu na Kaliani pamoja na ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Kigezi.

"Mama Samia hakuishia hapo kwenye elimu pia ameipandisha hadhi shule ya Sekondari Nyeburu, na sasa ina kidato cha kwanza mpaka cha sita. 

Haya ni matunda ambayo Mhe. Rais ameyafanya, sisi tumpongeze kwa kazi hii kubwa iliyotukuka na sisi tunamuombea dua Mungu aendelee kumuweka na kumjalia afya njema." Amesema Bw. Mambo.

Katika hatua nyingine, mwananchi huyo pia ameeleza kuhusu urahisi wa sasa wa wananchi kupata Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kupitia programu maalumu iliyoanzishwa ngazi ya Kata pamoja na kasi ya ujenzi wa tenki kubwa la maji Bangulo, akisema yote hayo ni sehemu ya jitihada za serikali za kuondoa changamoto zote zinazowakwaza wananchi.

Ameeleza pia kuhusu fursa za uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia Mikopo ya Halmashauri inayotolewa kwa Vijana, wanawake na wenye ulemavu, akisisitiza wajibu wa kila mmoja kulinda amani ili kuruhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ustawi wa wananchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com