Na Sumai Salum – Kishapu
Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imeendelea kuonesha mafanikio makubwa katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020–2025, baada ya kufikia asilimia 48.9 ya utekelezaji katika kipindi cha Julai hadi Disemba 2025.
Taarifa hiyo imewasilishwa Januari 21, 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi, wakati wa kikao cha Halmashauri kuu ya CCM Wilaya, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Chama hicho Wilaya ya Kishapu.
Akitoa taarifa hiyo, Mhe. Masindi amesema kuwa utekelezaji huo umetokana na ushirikiano mzuri kati ya Serikali, Chama Cha Mapinduzi pamoja na wananchi, hali iliyopelekea kukusanywa na kutekelezwa jumla ya shilingi bilioni 5.13, sawa na asilimia 48.9 ya makisio ya shilingi bilioni 10.50 yaliyopangwa kwa kipindi husika.
UTEKELEZAJI KWA SEKTA MUHIMU ZA MAENDELEO
Katika Sekta ya Afya, Wilaya ilipokea shilingi 575,000,000, ambapo hadi Disemba 2025 kiasi cha shilingi 296,984,829.84 kilikuwa kimepokelewa na kutekelezwa, fedha zilizolenga kuboresha huduma za afya na miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za tiba.
Kwa upande wa Sekta ya Elimu, jumla ya shilingi 3,978,709,752.60 zilipokelewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu, ambapo hadi Disemba kiasi cha shilingi 1,697,654,000 kilikuwa kimepokelewa na kutumika katika ujenzi wa madarasa, vyoo, nyumba za walimu pamoja na ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia.
Sekta ya Kilimo, Wilaya ilipokea shilingi 72,827,836.30, fedha zilizotumika kuimarisha huduma za ugani, kuongeza uzalishaji na kuwajengea uwezo wakulima ili kuongeza tija na kipato chao.
Sekta ya Biashara na Uwekezaji, Wilaya ilifanikiwa kukusanya shilingi 310,694,325.00, fedha zilizotumika kuboresha mazingira ya biashara, kuongeza ajira na kukuza uchumi wa wananchi.
Aidha, kupitia Sekta ya Maendeleo ya Jamii, jumla ya shilingi 304,000,000 zilitolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia mikopo ya asilimia 10, hatua iliyochangia kuinua uchumi wa kaya na makundi maalum.
Kwa upande wa Sekta ya Umeme, kiasi cha shilingi 289,193,967.36 kilitumika kupeleka na kuboresha huduma ya umeme katika maeneo ya vijijini na mijini, jambo lililorahisisha shughuli za uzalishaji na huduma za kijamii.
Sekta ya Barabara, Wilaya ilipokea shilingi 1,908,563,308.00, fedha zilizotumika katika ujenzi na matengenezo ya barabara ili kuboresha miundombinu ya usafiri na kurahisisha shughuli za kiuchumi ndani ya wilaya.
Pia Sekta ya Maji,Wilaya ilipokea kiasi cha shilingi 387,391,711.98 kwa ajili ya utekelezaji miradi mbalimbali ya maji ndani ya Wilaya na Kata
Mwenezi CCM Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Jiyenze Seleli akizungumza kwenye kikao hicho
Hata hivyo, Mhe. Masindi amewahimiza viongozi wa CCM na watendaji wa Serikali kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi kwa uadilifu na uwajibikaji, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na wananchi ili kuhakikisha malengo ya Ilani ya CCM yanafikiwa kikamilifu.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kishapu, Shija Ntelezu, amesema Chama kimeridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM kwa kipindi cha Julai hadi Disemba 2025.
"Taarifa hii inaonesha wazi kazi kubwa inayofanywa na Serikali chini ya usimamizi wa Mkuu wa Wilaya kwa kushirikiana na watendaji na wananchi. Tunawapongeza viongozi na watendaji wote kwa kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hususan katika sekta za elimu, afya, barabara na kilimo. Ni wajibu wetu kama Chama kuendelea kusimamia, kuhimiza uwajibikaji na kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa viwango vinavyokubalika.”ameongeza Ntelezu
Aidha, amewahimiza wajumbe wa CCM kuendelea kuwa mabalozi wa utekelezaji wa Ilani ya Chama kwa wananchi, kwa kusikiliza kero, kutoa elimu na kuimarisha mshikamano kuelekea kukamilika kwa kipindi cha utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Social Plugin