Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

GHARAMA YA MACHAFUKO IRAN: FUNZO KWA WACHOCHEZI WA KIDIJITALI NA USALAMA WA MATAIFA

Gharama ya machafuko ya kisiasa na kijamii imezidi kuwa kubwa kwa raia wa kawaida nchini Iran ambapo kwa sasa taifa hilo limeingia katika majonzi mazito kufuatia vifo vya maelfu ya watu vilivyotokea katika kipindi cha wiki chache zilizopita. 

Hali hii inatoa taswira halisi kuwa kuhamasisha vurugu kupitia majukwaa ya kidijitali ni jambo rahisi linaloweza kufanywa na mtu yeyote akiwa nyuma ya kioo cha simu au kompyuta, lakini matokeo yake mtaani yanatisha kwa kusababisha vifo, ulemavu na uharibifu wa miundombinu ambayo imechukua miongo kadhaa kuijenga. Ni ukweli usiopingika kuwa amani ni gharama nafuu zaidi kuliko ukombozi wowote unaotafutwa kupitia njia ya umwagaji damu na vurugu za barabarani ambazo mara nyingi huacha makovu yasiyofutika kwa vizazi vingi.

Katika kile kinachoonekana kama mabadiliko ya msimamo wa kijiopolitiki, Rais wa Marekani Donald Trump ameanza kurudi nyuma katika ahadi zake za kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya utawala wa Iran licha ya hapo awali kuwaahidi waandamanaji kuwa msaada ulikuwa njiani. 

Hatua hii ya Trump inaonyesha wazi jinsi mataifa makubwa yanavyoweza kutoa matumaini ya mabadiliko kupitia kauli za kisiasa, lakini yanapokutana na uhalisia wa gharama za vita na maslahi ya kikanda, mara nyingi huamua kutumia diplomasia ya siri na kuwaacha raia waliokuwa barabarani baada ya kuchjochewa kisaikolojia wakikabiliana na mkono wa chuma wa vyombo vya usalama. Hii ni fundisho kubwa kwa wanaharakati wa kidijitali nchini Tanzania na kwingineko duniani kuwa kutegemea nguvu za nje kuleta mabadiliko ya ndani ni sawa na kutegemea kivuli kukulinda na jua, kwani mataifa hayo yataangalia maslahi yao kwanza kabla ya usalama wa raia wa nchi nyingine.

Maumivu na majonzi yanayotanda nchini Iran hivi sasa yanapaswa kuwa chati ya tahadhari kwa kila anayetumia mitandao ya kijamii kueneza chuki au uchochezi wa vurugu, kwani moto unaowashwa kidijitali huunguza watu halisi na mali zao katika ulimwengu wa nyama na damu. Ni wajibu wa kila mwananchi kutambua kuwa amani iliyopo ni tunda la busara, na kuichezea ni sawa na kualika majanga ambayo gharama yake ni kubwa kuliko faida yoyote ya kisiasa inayotafutwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com