Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DUNIA INATUTAMBUA: TUSICHEZE NA MAGEUZI YA KIDIJITI KWA SIASA ZA "KIKARATASI"





KATIKA kipindi ambacho Tanzania inazidi kupaa kimataifa, Ripoti ya hivi karibuni ya Benki ya Dunia (2025) imeweka muhuri wa dhahabu: Tanzania sasa ni miongoni mwa mataifa kinara duniani (Kundi A) katika ukomavu wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Mafanikio haya si ya bahati mbaya; ni matokeo ya uwekezaji mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kujenga Serikali Mtandao (e-GA). Lakini wakati dunia ikitupigia makofi kwa kupanda kutoka nafasi ya 90 hadi ya 26 duniani, kuna somo kubwa kwetu: Tusikoroge mafanikio haya kwa ubaguzi au mitazamo finyu ya kisiasa.

Mageuzi haya ya kidijiti ndiyo yanayotoa uhalali wa uanzishwaji wa Jukwaa la Vijana Tanzania (Youth Platform Tanzania). Jukwaa hili si la "kuchora" wala la "hadithi," bali ni nyenzo ya kisasa inayotumia mfumo wa kidijiti kuunganisha vijana na serikali yao.

Katika ulimwengu wa sasa, kijana wa Mwanza, Mbeya, au Lindi hahitaji kusubiri mchakato mzito wa "Baraza la Kisheria" uliokwama kwenye makaratasi tangu mwaka 2015. Anahitaji jukwaa la kidijiti ambalo ni fast-track, linalomwezesha kuwasilisha kero yake na kupata suluhu papo hapo kupitia mifumo kama e-Mrejesho ambayo Benki ya Dunia imeisifu.

Hoja ya ACT: Je, Tunataka Sheria au Matokeo?

Hapa ndipo hoja ya Ngome ya Vijana ya ACT Wazalendo inapoonekana kukosa mashiko katika kasi ya sasa. Wakati dunia inatutambua kwa "Ukomavu wa Kidijiti" na "Utoaji wa Huduma," wenzetu bado wanang’ang’ania taratibu za kisheria zinazochelewesha mambo.

Hoja kuwa jukwaa hili halina sheria ni sawa na kumkataza mtu kutumia simu janja (smartphone) kwa sababu tu bado sheria ya simu za mezani haijarekebishwa. Dunia haitusubiri! Kasi ya Waziri Joel Nanauka na serikali kwa ujumla ni kasi ya matokeo. Vijana wanataka ajira, wanataka mikopo, na wanataka kusikilizwa—mambo ambayo Jukwaa la Vijana linatekeleza kwa kutumia mifumo ile ile iliyotufanya tuwe vinara Afrika Mashariki.

Mafanikio haya ya TEHAMA yanapaswa kutumika kuunganisha taifa, siyo kubomoa. Ni hatari kutumia majukwaa ya kidijiti kutoa taarifa za kukatisha tamaa au kupinga juhudi za serikali kwa sababu tu za kiu ya "Kiki" ya kisiasa.

Tanzania imeshika nafasi ya pili Afrika baada ya Mauritius. Hii ni heshima kubwa! Tunapozindua majukwaa kama haya ya vijana, tunadhihirisha kuwa "Serikali Mtandao" si kwa ajili ya kulipa kodi tu, bali ni kwa ajili ya kuwashirikisha wananchi (Citizen Engagement).

Wito kwa Vijana Tusirudi nyuma. Dunia inatutazama kama mfano wa kuigwa. Jukwaa la Vijana ni fursa ya dhahabu inayotumia miundombinu ile ile iliyosifiwa na Benki ya Dunia. Badala ya kupoteza muda kubishana kuhusu "vifungu vya sheria" vinavyoweza kurekebishwa mbeleni, vijana tuitumie fursa hii kuingia kwenye mfumo, kuwasilisha hoja zetu, na kuijenga Tanzania.

Ukweli unabaki palepale: Tanzania ni yetu, na sasa inang’ara kidijiti. Tusikubali siasa za kizamani zitupotezee mwelekeo wa maendeleo ya kisasa. Tuyajenge ya Tanzania, dunia ishatatambua!

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com