Mbunge viti maalum Tunduru Sikudhani Yassin Chikambo akiwa na meneja wa TARURA Wilaya ya Tunduru Mhandisi Kweka wakiwa wanakagua kivuko cha Masonya chenye changamoto kubwa kwa wakazi wa maeneo hayo
Na Regina Ndumbaro Tunduru-Ruvuma
Mbunge wa viti maalumu kutoka Wilaya ya Tunduru, mheshimiwa Sikudhani Yassin Chikambo amefanya ziara ya kukagua miundombinu korofi katika kata ya Masonya akiwa ameongozana na meneja wa TARURA Wilaya ya Tunduru, Mhandisi Kweka.
Ziara hiyo imelenga kujionea changamoto zinazowakabili wananchi, hususani katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha mara kwa mara wilayani humo.
Katika ziara hiyo Sikudhani Chikambo ametembelea kivuko cha Masonya ambacho kimekuwa kero kubwa kwa wakazi na wakulima wa kata hiyo.
Kivuko hicho kimeripotiwa kusababisha madhara makubwa kwa wananchi, hasa wakati wa mvua nyingi, hali inayokwaza shughuli za kiuchumi na usafiri wa wakazi wa eneo hilo.
Aidha, pia Chikambo ametembelea kijiji cha Nakayaya Mashariki (Misufini) ambako kuna changamoto kubwa ya barabara inayokatiza katika bonde hatarishi.
Bonde hilo limeendelea kupanuka kutokana na mvua za mara kwa mara, hali inayohatarisha usalama wa wananchi na kuathiri mawasiliano ya barabara katika eneo hilo.
Chikambo ameambatana na katibu wa siasa na uenezi wa CCM wilaya ya Tunduru, Komredi Yanini Stambuli, pamoja na diwani wa kata ya Masonya, Saidi Bwanali.




Social Plugin