Na Mwandishi wetu, Dodoma
Hatimaye wananchi waliokuwa wakihofia gharama za matibabu wanaanza kuona mwanga, baada ya Serikali kutangaza kuanza kwa awamu ya kwanza ya Bima ya Afya kwa Wote, mpango unaolenga kulinda haki ya msingi ya kupata huduma za afya bila kuangalia uwezo wa kifedha.
Awamu hii inalenga moja kwa moja makundi yaliyo hatarini zaidi, wakiwemo wazee, watoto, wanawake wajawazito na watu wenye ulemavu, ambao gharama zao zitabebwa na Serikali.
Katika awamu hii, Serikali imeanza rasmi utekelezaji wa Kitita cha Huduma Muhimu chenye thamani ya shilingi 150,000 kwa kaya isiyozidi watu sita, huku makundi yasiyo na uwezo yakigharamiwa bila kulipa chochote.
Akizungumza leo January 23,2026 jijini Dodoa kwenye kikao kazi cha kujadili utekelezaji wa bima ya afya kwa Wote waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa amesema huduma zitapatikana katika vituo vya afya vilivyosajiliwa kwa kufuata mfumo wa rufaa, kuanzia tarehe 26 Januari 2026, hatua inayotarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa mzigo wa kifedha kwa familia nyingi.
Mchengerwa, amesema afya ni msingi wa maendeleo ya Taifa, akisisitiza kuwa hakuna mabadiliko ya kweli yanayoweza kudumu endapo wananchi wake ni dhaifu kiafya. Alieleza kuwa Bima ya Afya kwa Wote ni uwekezaji wa kimkakati katika utu wa Mtanzania na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Grace Magembe, amesema utekelezaji wa mpango huo ni hatua ya kihistoria inayobadilisha dhana ya huduma za afya kutoka kuwa mzigo binafsi hadi kuwa jukumu la pamoja la Taifa. Alibainisha kuwa awamu ya kwanza inalenga kuhakikisha makundi maalum yanalindwa dhidi ya gharama zinazoweza kuyasukuma kwenye umaskini.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, John Jingu, amesema mafanikio ya Bima ya Afya kwa Wote yatategemea kwa kiasi kikubwa uelewa wa wananchi. Alisisitiza kuwa wataalam wa maendeleo ya jamii wana wajibu wa kujenga fikra chanya na kuhamasisha ushiriki wa wananchi ili mpango huo uwe suluhu ya kudumu ya changamoto ya gharama za matibabu na kichocheo cha ustawi wa jamii.



Social Plugin