
Na OWM – TAMISEMI, Mwanza
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amesema Serikali kupitia Mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) imetumia kiasi cha bilioni 67 kujenga Barabara na Masoko ili kuwahudumia wananchi wa Mwanza.
Prof. Shemdoe ametoa taarifa hiyo leo jijini Mwanza wakati alipopewa nafasi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ya kuzungumza na wananchi wa mwanza waliojitokeza kumsikiliza Waziri Mkuu mara baada ya Waziri Mkuu kuhitimisha ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo na kuzindua meri ya New MV Mwanza.
Prof. Shemdoe amefafanua kuwa, fedha hizo zinatumika kujenga barabara ya Nyamaghani yenye urefu wa kilomita 14 yenye thamani ya bilioni 22, barabara ya Ilemela yenye urefu wa kilomita 12 yenye thamani ya bilioni 24, Soko la Samaki Mkuyuni Nyamaghana lenye thamani ya bilioni 7 pamoja na soko la mazao mchanganyiko Ilemela lenye thamani ya bilioni 14.
Akizungumzia hatua ya ujenzi wa barabara hizo, Prof. Shemdoe amesema zimekamilika na ziko kwenye hatua ya kuweka taa za barabarani ili wananchi waweze kuzitumia nyakati za usiku huku wakiwa salama.
“Mhe. Waziri Mkuu ikikupendeza pindi barabara zikikamilika, tutakuomba uje kuzizindua rasmi kwa ajili ya kuanza kutumiwa na wananchi wa Mwanza na watanzania wote watakao kuja jijini Mwanza kwa shughuli mbalimbali,” Prof. Shemdoe amewasilisha ombi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amemhakikishia Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa, ofisi yake itaisimamia vema TARURA ili miradi yote ya Barabara, Soko la Samaki na Soko la Mazao mchanganyiko ikaamilike kwa wakati, na hatimaye wanachi waanze kunufaika na uwepo wa miradi hiyo.



Social Plugin