Na Sumai Salum – Kishapu
Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga limefanya kikao chake cha kawaida cha pili leo Januari 28, 2026, kikilenga kupokea na kujadili taarifa za maendeleo kwa kipindi cha robo ya pili Oktoba-Disemba 2025/2026.
Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, madiwani wampata fursa ya kujadili mada mbalimbali za maendeleo ya Halmashauri hiyo sambamba na taarifa za kamati mbalimbali za kudumu.
Akizungumza kwa niaba ya Madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Mhe. Josephat Limbe, amesema Baraza la Madiwani limeazimia kwa pamoja kuchukua hatua za kukata mfumo wa mnunuzi mmoja wa zao la pamba katika Kata mbalimbali za wilaya hiyo, hatua inayolenga kufungua soko huria ili wakulima wanufaike zaidi na zao lao.
"Mfumo wa mnunuzi mmoja umekuwa ukilalamikiwa na wakulima kutokana na changamoto za bei ndogo na kukosa ushindani, hali inayowanyima fursa ya kupata thamani halisi ya mazao yao. Baraza linaamini kuwa kuwepo kwa soko huria kutawapa wakulima uhuru wa kuchagua wanunuzi, kuongeza ushindani na hatimaye kuinua kipato cha wananchi" ameongeza Mhe. Limbe.
Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa maamuzi hayo yanaonesha dhamira ya dhati ya Baraza la Madiwani katika kusimamia maslahi ya wananchi na kuhakikisha sekta ya kilimo, hususan zao la pamba, linaendelea kuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya kiuchumi kwa Wilaya ya Kishapu.
Akizungumza katika kikao hicho, Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Mhe. Lucy Thomas Mayenga, amewapongeza madiwani kwa mjadala mpana, wa kina na wenye tija kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo, akisema hatua hiyo inaakisi uwajibikaji wao kwa wananchi na dhamira ya dhati ya kuwatumikia.
Mhe. Mayenga amesisitiza kuwa Baraza la Madiwani lina nafasi muhimu katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi katika kata mbalimbali zinapatiwa ufumbuzi wa haraka kupitia ushirikiano wa karibu kati ya madiwani, wataalamu wa Halmashauri na Serikali Kuu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi akizungumza katika kikao hicho na kutoa msisitizo juu ya umuhimu wa kuimarisha masuala ya lishe mashuleni, akieleza kuwa lishe bora ni msingi wa maendeleo ya elimu, afya na ustawi wa watoto.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya huyo pia amesisitiza utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Watu Wote, akiwataka madiwani kuhamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya ili kupunguza gharama za matibabu na kuongeza upatikanaji wa huduma bora za afya kwa familia na jamii kwa ujumla.
Katika kikao hicho, Kamati za Kudumu zilizowasilisha taarifa zake ni pamoja na Kamati ya Kudhibiti UKIMWI, Kamati ya Huduma za Jamii, Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira pamoja na Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango.
Kikao hicho kimehitimishwa kwa wito wa Madiwani na wataalamu kuibua vyanzo vipya vya mapato, ukusanyaji wa mapato na kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya viongozi, wataalamu na wananchi, ili kuhakikisha kasi ya maendeleo inaendelea kuongezeka katika Wilaya ya Kishapu.
Social Plugin