Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA NISHATI , MAKAMBA APONGEZA MIRADI YA UMEME SHINYANGA


Naibu Waziri wa Nishati na Mbunge wa Viti Maalum mkoani Shinyanga, Mhe. Salome Makamba, ametembelea miradi mbalimbali ya nishati ya umeme ikiwemo kituo cha kupoza umeme cha Ibadakuli kilichopo Manispaa ya Shinyanga pamoja na mradi wa umeme wa jua uliopo Kijiji cha Ngunga wilayani Kishapu.

Mhe. Makamba amefanya ziara hiyo leo Januari 9, 2026, akiwa ameambatana na viongozi wa Serikali na Chama, ambapo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta ya nishati ya umeme.

Akizungumza mara baada ya kukagua miradi hiyo, amesema uwekezaji unaoendelea katika uzalishaji na usambazaji wa umeme utaifanya Tanzania kuwa na umeme wa kutosha, wa uhakika na wenye uwezo wa kuuzwa hata kwa nchi jirani.

“Leo nimeshuhudia uwekezaji mkubwa sana katika sekta ya nishati ya umeme. Nchi itazalisha umeme mwingi, tutakuwa na umeme wa uhakika, na tutaweza kuuza hata nchi jirani kama Uganda na Kenya, sambamba na kuhudumia miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo reli ya SGR,” amesema Makamba.

Aidha, amesisitiza kuwa katika utekelezaji wa miradi hiyo, wazawa hususan vijana wa maeneo yanayozunguka miradi hiyo wapewe kipaumbele cha ajira ili wanufaike kiuchumi.

“Nataka kuona vijana wengi wa Shinyanga wakipata ajira kwenye miradi hii ya nishati ya umeme. Hili si ombi, bali ni takwa la kisheria,” amesisitiza Makamba.

Pia amewataka vijana wanaopata ajira katika miradi hiyo kufanya kazi kwa uaminifu, kuzingatia uzalendo na kuepuka vitendo vya wizi wa vifaa vya ujenzi ambavyo vinaweza kuhatarisha utekelezaji wa miradi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Richard Masele, amemshukuru Rais Samia kwa uwekezaji huo wa nishati ya umeme akisema utachochea ukuaji wa uchumi wa mkoa na kuvutia wawekezaji zaidi.

Naye Kaimu Mkurugenzi Msimamizi wa Miradi wa TANESCO Makao Makuu, Mhandisi Frank Mashalo, amesema mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Ibadakuli unatekelezwa kwa ufadhili wa Serikali kwa asilimia 100, umefikia asilimia 43 ya utekelezaji na unagharimu Shilingi bilioni 25.

Akizungumza kuhusu mradi wa umeme wa jua, Msimamizi wa Mradi huo, Mhandisi Emmanuel Anderson, amesema awamu ya kwanza ya mradi imefikia asilimia 89 ya utekelezaji, ikizalisha Megawati 50 za umeme, na kwamba vijana wazawa 560 wameajiriwa, wakiwemo 67 kutoka Kijiji cha Ngunga kinachozunguka eneo la mradi.
Naibu Waziri wa Nishati Salome Makamba akizungumza.
Naibu Waziri wa Nishati Salome Makamba akizungumza.
Kaimu Mkurugenzi msimamizi wa miradi TANESCO Makao Makuu Mhandisi Frank Mashalo.
msimamizi wa umeme Jua Mhandisi Emmanuel Anderson akizungumza.
Mwenezi wa CCM Mkoa wa Shinyanga Richard Masele akizungumza.
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Samweli Jackson akizungumza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com