Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MFUMO WA KIDIGITALI PSSSF KIBOKO YA MATAPELI WA WASTAAFU


Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umesema kuimarika kwa mifumo yake ya kidigitali kumeleta mwarobaini wa vitendo vya utapeli ambavyo vimekuwa vikiwalenga wastaafu wa mfuko huo nchini.

​Hayo yamebainishwa Januari 22, 2026 wilaya ya Musoma mkoani Mara na mtoa mada kutoka PSSSF, Bw. Nuru Mahinya, wakati wa semina maalum iliyotolewa kwa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara (MRPC) yenye lengo la kuwajengea uwezo wanahabari kuhusu utendaji wa mfuko.
Bw. Mahinya amesema kuwa mfumo huo mpya unamwezesha mwanachama kuanzia mchakato wa dai lake na kulifuatilia hatua kwa hatua kupitia simu yake ya kiganjani, jambo linaloziba mianya ya watu wa kati au matapeli kujipenyeza.

​"Lengo la mfumo huu ni pamoja na kupunguza utapeli. Sasa hivi tapeli akikupigia simu, mwambie kila kitu nakiona kupitia simu yangu ya kiganjani. Kuanzia kuanzisha dai, mwanachama anaweza kufuatilia hatua kwa hatua kuanzia kwa mwajiri hadi dai linapofika kwenye mfuko," alisema Bw. Mahinya.

​Naye Afisa Uhusiano na Elimu kwa Wanachama Mwandamizi wa PSSSF, Bi. Rehema Mkamba, alifafanua kuwa mapinduzi hayo ya kidigitali yamesaidia kuongeza uwazi na kupunguza usumbufu wa wanachama kufuata huduma maofisini.
​"Mfumo huu unasaidia wanachama kulipwa kwa uwazi, kwa wakati na bila usumbufu. PSSSF inashukuru kwa ushirikiano huu na MRPC, na tunaamini huu ni mwanzo mzuri wa kuhakikisha elimu sahihi inawafikia wanachama wetu," alisema Bi. Mkamba.

​Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MRPC, Bw. Jacob Mugini aliushukuru uongozi wa PSSSF kwa kutoa mafunzo hayo akidai kuwa yamefungua uelewa wa mambo mengi ambayo awali yalikuwa hayafahamiki vizuri.

"Sasa tutakuwa mabalozi wazuri wa PSSSF kwa kutumia vyombo vyetu kuelimisha umma. Elimu hii imetusaidia kufahamu mambo mengi ambayo yatakuwa na faida kubwa kwa wastaafu wetu mkoani Mara," alisema Bw. Jacob.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com