Na Mwandishi Wetu Malunde 1-Blog
Mheshimiwa Dkt. Juma Zuberi Homera, Waziri wa Katiba na Sheria, amewasili nchini Kenya kuongoza kikao cha Mawaziri wa Sheria na Haki wa Umoja wa Afrika (AU).
Kikao hicho kinawakutanisha mawaziri kutoka nchi wanachama wa AU kwa lengo la kujadili masuala muhimu ya kisheria na haki, pamoja na kuweka mwelekeo wa pamoja unaolenga kuimarisha mifumo ya sheria barani Afrika.
Lengo kuu la kikao hicho ni kuimarisha mifumo ya kisheria ya nchi wanachama, kufanya mapitio ya sheria mbalimbali na kuweka mikakati ya pamoja ya kulinda maslahi ya bara la Afrika katika majukwaa ya kimataifa.
Vilevile, kikao hicho kinalenga kuendeleza mshikamano, ushirikiano wa kisheria na kubadilishana uzoefu katika masuala ya haki, utawala bora na utawala wa sheria miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika.
Ushiriki wa Tanzania katika kikao hiki unaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kulinda na kutetea maslahi ya Taifa na ya bara la Afrika kwa ujumla.
Dhamira hiyo inaakisi msimamo thabiti wa Tanzania katika kuimarisha sheria, haki, utawala bora na kuendeleza ushirikiano wa kikanda na kimataifa.



Social Plugin