Mkazi wa Mwasele “B” wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Suzan Shagembe, akizungumzia hatua zilizochukuliwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Peter Masindi, za kuagiza mashimo na visima vyote vilivyowazi kufukiwa au kufunikwa ili kuepukana na vifo vya watoto
Na Sumai Salum – Kishapu
Wananchi wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wamepongeza hatua zilizochukuliwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Peter Masindi, za kuagiza mashimo na visima vyote vilivyowazi kufukiwa au kufunikwa mara moja, hatua inayolenga kuzuia vifo na majeruhi vinavyotokana na mashimo hayo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wamesema uwepo wa mashimo mengi yaliyotelekezwa hasa maeneo ya makazi umeendelea kuwa tishio kubwa kwa usalama wa watoto na hata watu wazima.
Mkazi wa Mwasele “B”, Suzan Shagembe, amesema agizo hilo ni la msingi na linapaswa kusimamiwa kwa nguvu zote kwani mashimo mengi yamekuwa chanzo cha vifo vya watoto wanaocheza karibu nayo.
“Watoto wengi wamepoteza maisha kwa kuanguka kwenye mashimo haya. Hii ni hatua kubwa na ya kupongezwa kwa Mkuu wa Wilaya kwa kuamua kulikabili tatizo hili moja kwa moja,” amesema Suzan.
Ameongeza kuwa hatari hiyo haiwaathiri watoto pekee, bali hata watu wazima, hususani walevi au wageni wasioufahamu vizuri mazingira ya eneo husika.
“Unakuta mtu ni mlevi au mgeni wa eneo, anadumbukia kwenye shimo na kupata ulemavu au hata kupoteza maisha. Hili ni tatizo hatari sana,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mussa John Kisinza mkazi wa Beledi amesema hatua hiyo itasaidia kurejesha uwajibikaji kwa jamii, hasa kwa watu wanaochimba mashimo bila kuchukua tahadhari za usalama.
Naye Juliana Charles wa Mwasele “B” amesema ni wakati muafaka sasa kwa wananchi kushirikiana na viongozi wa maeneo yao kuhakikisha mashimo yote yanatambuliwa na kuchukuliwa hatua stahiki.
Agizo la kufukia au kufunika mashimo lilitolewa na Mhe. Masindi mapema wiki iliyopita wakati akizungumza kwenye kikao cha tathmini ya lishe kwa kipindi cha Julai–Septemba, akisisitiza kuwa watoto wamekuwa waathirika wakubwa wa mashimo yasiyozibwa.
Katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya pia aliwakumbusha wazazi kuacha mara moja tabia ya kuwapeleka watoto chini ya miaka 18 kuchunga mifugo, akibainisha kuwa watoto hao hawawezi kujilinda pindi wanapokutana na hatari mbalimbali ikiwemo wanyama wakali kama fisi au kuvuka mito.
“Jamii yetu imepoteza watoto kwa sababu ya mashimo yasiyofukiwa huu ni uzembe, ninaagiza na viongozi wa Kata na Vijiji wahakikishe Kila aliyechimba shimo afukie mara moja, au alifunikie kwa vifaa imara, aweke uzio na alama za onyo. Kuanzia leo, shimo lolote linalobaki wazi litaripotiwa kwa viongozi wa mtaa na mwenye shimo atawajibika.”
“Msimu wa mvua umeanza, na mashimo yaliyowazi ni hatari kubwa kwa watoto. Tuchukue hatua sasa: fukia au funika, weka uzio na onyo ili kulinda uhai wa watoto wetu likiwa ni jukumu la kila mmoja,” amesisitiza.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa Wilaya ya Kishapu wa kuimarisha usalama wa wananchi, hususan watoto, na kuzuia vifo vinavyoweza kuepukika kwa kuchukua tahadhari mapema.

Mkazi wa Beledi wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Mussa John Kisinza, akizungumzia hatua zilizochukuliwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Peter Masindi, za kuagiza mashimo na visima vyote vilivyowazi kufukiwa au kufunikwa ili kuepukana na vifo vya watoto
Mkazi wa Mwasele “B” wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Juliana Charles Ngassa, akizungumzia hatua zilizochukuliwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Peter Masindi, za kuagiza mashimo na visima vyote vilivyowazi kufukiwa au kufunikwa ili kuepukana na vifo vya watoto

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Peter N. Masindi akizungumza




Mkazi wa Beledi wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Mussa John Kisinza, akizungumzia hatua zilizochukuliwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Peter Masindi, za kuagiza mashimo na visima vyote vilivyowazi kufukiwa au kufunikwa ili kuepukana na vifo vya watoto
Mkazi wa Mwasele “B” wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Juliana Charles Ngassa, akizungumzia hatua zilizochukuliwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Peter Masindi, za kuagiza mashimo na visima vyote vilivyowazi kufukiwa au kufunikwa ili kuepukana na vifo vya watoto
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Peter N. Masindi akizungumza
Social Plugin