Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Saa nane usiku, Mariam Mahinyila, mkazi wa Dodoma, huamka akiwa amelowa jasho jingi,mwili wake ukiwa unatetemeka, moyo unadunda kwa kasi, na usingizi unakatika ghafla.
Kila usiku ni vita ya kimya kimya anayopambana nayo peke yake, bila kuelewa kwa nini maisha yake yamebadilika ghafla.
Mariam alianza kubadilika taratibu,kwanza ilikuwa ni kusahau vitu vidogo kazini, kisha uchovu wa mara kwa mara, baadaye hasira zisizoelezeka na kukosa usingizi.
Nyumbani hali ilianza kuwa tofauti,mazungumzo na mume wake yakapungua, na kila kosa dogo likawa chanzo cha ugomvi mkubwa baina yao.
Baada ya miezi kadhaa, mume wake alianza kumtazama kwa macho ya mashaka. “Huyu si yule Mariam niliyemuoa miaka 35 iliyopita,” mguso wa upendo ulianza kupotea, na nyumba iliyokuwa na furaha sasa ikajaa ukimya na mashaka.
Lakini Mariam mwenyewe hakuelewa kinachoendelea mwilini mwake alianza kuhisi kama amepoteza thamani ndani ya nyumba yake mwenyewe.
Kazini, hali ni mbaya zaidi,Mariam amekuwa akisahau mambo madogo madogo, anakosa umakini, na mara kadhaa amepewa onyo la maandishi kuhusu kuporomoka kwa utendaji wake. Kila siku anaishi na hofu ya kupoteza ajira.
Lakini ukweli anaoukabili si ugonjwa wa ajabu wala laana,ni menopause, yaani kipindi cha kukoma hedhi hatua ya kawaida ya maisha ambayo jamii imeamua kuipuuza na kuifunika kwa ukimya.
Baada ya ushauri wa kitabibu, alifanyiwa uchunguzi hospitalini na kugundulika kuwa alikuwa katika hatua ya kukoma hedhi.
Kwa lugha ya kitaalam, menopause ni mabadiliko ya kawaida ya kibaolojia, lakini yanayoathiri maisha yake kwa kiwango kikubwa kuliko alivyowahi kufikiria.
Mariam anaeleza;"Sikuwa najua kinachoendelea mwilini mwangu,nilianza kuhisi kama sipendwi tena nyumbani kwangu mwenyewe.”
Anasema hali hiyo imemfanya aone umuhimu wa elimu kuhusu menopause kuingizwa kwenye programu za afya ya uzazi, kuanzishwa kwa huduma maalum kwa wanawake wa umri wa kati, pamoja na kampeni za kitaifa za uelimishaji ili kupunguza unyanyapaa.
Hali hiyo huwapata wanawake wengi si Mariam peke yake, wengi hupitia hali hii kimya kimya bila msaada.
Nzuwa Njilimuhi, mwalimu wa shule ya msingi Chinusi wilayani Mpwapwa, mkoani Dodoma, mwenye umri wa miaka 49, naye anapitia hali kama hiyo lakini kwa namna yenye maumivu tofauti.
Anasimulia kuwa akiwa darasani hukosa umakini ghafla, husahau alichokuwa akifundisha, na wakati mwingine hukasirika mbele ya wanafunzi bila sababu za msingi, hali iliyosababisha hata kuwapa adhabu zisizostahili.
Anasema hali hiyo imemletea aibu na fedheha kubwa kazini na hofu ya kudharauliwa na wanafunzi na walimu wenzake.
“Wakati mwingine nahisi kama si mimi tena,najikuta nawachukulia watoto kwa ukali kupita kiasi, kisha najilaumu sana baadaye,” anasema kwa uchungu.
Lakini kilicho kigumu zaidi si darasa, bali maisha ya nyumbani.
Mabadiliko ya mwili wake yameanza kuathiri mahusiano yake na mume wake, ambaye wakati mwingine humtuhumu kuwa amebadilika au ana mahusiano mengine.
Kwa wanawake hawa wawili, menopause si tu suala la afya ni mzigo unaovuruga ndoa, kazi na hata heshima yao katika jamii.
Wataalamu wa afya ya wanawake na uzazi wanaeleza kuwa menopause hutokea pale ambapo mwanamke hukosa hedhi kwa miezi 12 mfululizo kutokana na kupungua kwa homoni za estrogen na progesterone.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi (Gynecologist) wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk. Mansour Mahmod anasema kwa kawaida hutokea kati ya umri wa miaka 45 hadi 55, ingawa inaweza kuanza mapema au kuchelewa kutokana na sababu mbalimbali za kiafya.
Anaeleza kuwa kupungua kwa homoni hizo husababisha joto la ghafla mwilini, jasho la usiku, usingizi hafifu, uchovu wa mara kwa mara, mabadiliko ya hisia na kupungua kwa umakini.
"Athari zake haziishii mwilini pekee zinaingia moja kwa moja kwenye uchumi wa familia,wanawake wengi katika umri huu bado ni nguzo ya kipato cha familia wanapopitia dalili kali bila msaada, uzalishaji hupungua, ucheleweshaji huongezeka, na wengine hupoteza ajira,"anasema na kuongeza;
Hii huongeza mzigo kwa familia na wakati mwingine kuingiza kaya kwenye changamoto za kifedha.
Anasema kwenye ndoa, mabadiliko ya hisia na kupungua kwa hamu ya tendo la ndoa husababisha migogoro isiyoeleweka.
Wanaume wengi, wasio na elimu sahihi, hutafsiri hali hiyo kama mabadiliko ya tabia,kuchepuka au kupungua kwa upendo, jambo linaloleta umbali wa kihisia na wakati mwingine kuvunjika kwa ndoa.
Mtaalamu wa afya ya akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Dk. Veronica Lyimo, anaonya kuwa wanawake wanaopitia menopause bila msaada wako kwenye hatari ya msongo wa mawazo, huzuni na kujitenga na jamii.
Anaeleza kuwa mabadiliko ya mama nyumbani yanaweza kuathiri malezi, upendo na mazingira ya kujifunzia, jambo linaloacha alama ya muda mrefu kwa watoto.
Anaongeza kuwa licha ya ukubwa wa changamoto hizi, menopause bado ni mada inayozungumzwa kwa ukimya.
“Wanawake wengi huona aibu kuzungumza, wengine huamini ni sehemu ya kuzeeka, hivyo kutoona haja ya huduma za kitabibu,” anasema.
Anasema wanawake wa umri wa kati wanapopitia dalili kali bila msaada hupata kushuka kwa uzalishaji, kupoteza ajira, na kuongezeka kwa msongo wa maisha.
Kwa maneno mengine, menopause isiyoeleweka si suala la afya pekee bali ni mtikisiko wa uchumi wa nyumba unaoanza kimya kimya.
Madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi wanaeleza kuwa dalili za menopause hutofautiana kati ya mwanamke mmoja na mwingine.
Wanasema mwanamke anayepata dalili zinazoathiri maisha yake hapaswi kukaa kimya, bali anapaswa kufika kituo cha afya kwa uchunguzi na ushauri wa kitaalamu.
Pia wanaonya kuwa si kila dalili katika umri huo ni “kawaida,” kwani baadhi zinaweza kufanana na magonjwa mengine yanayohitaji matibabu.
Kwa mujibu wa Daktari Bingwa wa afya ya uzazi wa Hospitali ya Rufaa Dodoma Amina Ndogwe , menopause ni kukoma kabisa kwa hedhi kwa muda wa angalau miezi 12 mfululizo kutokana na kupungua kwa homoni za estrogen na progesterone.
Anaeleza kuwa perimenopause ni kipindi cha mpito kinachotangulia menopause ambapo hedhi hubadilika kabla ya kukoma kabisa.
"Kwa wastani, wanawake huingia menopause kati ya miaka 45 hadi 55, lakini inaweza kuanza mapema au kuchelewa kutokana na sababu mbalimbali,"anasema.
Anasema dalili za awali ni pamoja na hedhi isiyo ya kawaida, hot flashes, jasho la usiku, mabadiliko ya usingizi, uchovu na mabadiliko ya hisia.
Baadhi ya wanawake hupitia bila dalili kali, ingawa wengi hupitia changamoto za kiwango fulani.
Anasisitiza kuwa kupungua kwa estrogen huathiri mifupa, moyo na afya ya akili, na huongeza hatari ya osteoporosis na magonjwa ya moyo.
Katika familia nyingi, watoto huathirika bila kujielewa.
Mama anapopitia msongo au uchovu
malezi hubadilika kuwa ya hasira au ukimya,watoto hupoteza ukaribu wa kihisia,mazingira ya kujifunzia nyumbani huharibika na watoto hukua wakidhani mama wanaonewa.
Kwa mtazamo wa kijadi hususani kwa mila za kigogo, kukoma hedhi huonekana kama hatua ya heshima na ukomavu.
Chifu wa Kabila la Wagogo Mazengo wa Pili anasema mwanamke anapofikia hatua hii huheshimiwa zaidi na kuchukuliwa kama ni Mwanamke mwenye busara na kushauriwa kutumia virutubisho .
Katika mila hizo, lugha ya mafumbo hutumika kulinda staha, kama “kupumzika kwa maumbile” au “kufunga mlango wa damu ya uzazi.”
Menopause si mwisho wa maisha ya mwanamke, bali bila uelewa inaweza kuwa chanzo cha kuvunjika kwa ndoa, kuporomoka kwa uchumi wa familia na kuathiri watoto.
Kila Mariam anayepitia usiku wa maumivu kimya kimya anahitaji kueleweka, kusikilizwa na kusaidiwasio kuhukumiwa.
Kuvunja ukimya kuhusu menopause ni hatua ya kulinda familia, uchumi na heshima ya mwanamke katika jamii.




Social Plugin