Itigi, Singida
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Kati , leo Desemba 19, 2025 limetoa elimu kwa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi mkoani Singida, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha wafanyabiashara wanafanya shughuli zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na Matakwa ya viwango vilivyowekwa na Serikali kupitia Shirika.
Elimu hiyo imetolewa kufuatia mkataba wa mashirikiano uliopo kati ya TBS na Halmashauri zote nchini, unaolenga kusimamia jukumu la udhibiti ubora wa bidhaa za Chakula na Vipodozi, ufuatiliaji wa usajili wa bidhaa hizo pamoja na majengo ya yanayotumiwa kuuza biashara hizo za vyakula na vipodozi.
Jukumu hili lilikuwa likitekelezwa na taasi iliyokuwa inaitwa TFDA.
Hata hivyo, mabadiliko hayo yalikuwa hayajaeleweka vizuri kwa baadhi ya wafanyabiashara, hali iliyopelekea TBS Kanda ya Kati kuamua kutoa ufafanuzi wa kina kwa wadau husika.
Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu hiyo, Meneja wa TBS Kanda ya Kati, Bw. Hamisi Sudi Mwanasala, amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha wafanyabiashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi pamoja na Kata ya Mitundu kuelewa wajibu wao katika kusajili majengo ya biashara na kuhakikisha wanauza bidhaa za chakula na vipodozi zinazokidhi matakwa ya viwango vya ubora na zilizosajiliwa.
Bw. Mwanasala amesisitiza kuwa lengo kuu la TBS ni kuona kwamba inalinda afya na usalama wa jamii kwa kuuziwa bidhaa zenye ubora
Sambamba na hilo kuona kwamba wafanyabiashara waendeshe shughuli zao kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo ili kuepuka migogoro na mamlaka za udhibiti.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mitundu, Bi. Utukufu Gwimile, ameipongeza TBS kwa hatua ya kuamua kufika moja kwa moja kwa wafanyabiashara katika ngazi hadi ya kata na kutoa elimu hiyo, akisema kuwa kwa kufanya hivyo kumeondoa sintofahamu iliyokuwepo kwa wafanyabiashara walio wengi wa Kata ya Mitundu kuhusu utekelezaji wa kanuni za viwango ya mwaka 2021 inayosimamia kazi za TBS zinazofanywa na halmashauri.
Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Kata ya Mitundu, Bw. Moshi Hassan, amepongeza juhudi za TBS akisema kuwa wafanyabiashara wamefurahishwa sana na elimu waliyoipokea.
Ameongeza kuwa kuanzia sasa wafanyabiashara wako tayari kuzingatia sheria zote za viwango na kutii taratibu zilizopo bila kushurutishwa.
TBS Kanda ya Kati inayohudumia mikoa ya Dodoma, Singida na Iringa imeendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wafanyabiashara, halmashauri na taasisi za udhibiti ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na kuuzwa nchini zinakuwa zenye ubora na salama ili kuona kwamba afya na usalama wa walaji unatiliwa maanani.

















Social Plugin